Maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini - TAWA
kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Kahunda kilichopo Kata ya Katwe
Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema na mkoa wa Mwanza wamefanikiwa
kumdhibiti mamba aliyezua taharuki takribani wiki nzima Kijijini humo kabla ya
kuleta madhara Kwa binadamu.
Tukio la kumdhibiti mnyama huyo mkali na mharibifu lilitokea Oktoba 03, 2024 mara baada ya wananchi wa Kijiji hicho kutoa taarifa kwa
Maofisa wa TAWA Kanda ya ziwa kituo
kidogo cha Mwanza ambao walifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumdhibiti
mnyama huyo Kwa kumuua Kwa mujibu wa Sheria.
Wananchi wa Kahunda wamesema mamba huyo amekuwa akileta
taharuki takribani wiki nzima Kwa kukamata mifugo yao wakiwemo bata, kuku na
mbwa Katika mwalo wa Kijiji hicho na Kijiji cha zabaga hali ambayo ilikuwa
ikiwafanya waishi Kwa wasiwasi mkubwa na kushindwa kufanya shughuli za
kibinadamu Kwa amani katika ziwa hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Kahunda Bw. Athumani Wambura ameipongeza Serikali kupitia maofisa wa TAWA
kwa kufanikisha zoezi la kumdhibiti mamba huyo na jitihada zote zinazofanywa na
taasisi hiyo Kijijini humo ikiwa ni pamoja na hatua mbalimbali wanazochukua
Katika kulinda maisha ya wananchi wa wilaya ya Sengerema dhidi ya athari za
wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko.
"Niseme tu nawapongezeni sana hawa ndugu zangu wa
maliasili (TAWA) jambo walilolifanya ni kubwa kwa wananchi wetu, Kwa namna moja
au nyingine tumepata amani kwa kumdhibiti huyu mnyama ambaye ni tishio kubwa
sana. Kwa miaka ya hivi karibuni wanyama hawa wameweza kuua watu wetu zaidi ya watatu katika Kijiji cha Kahunda," amesema Athumani
Wambura.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho Kwa ushirikiano walioutoa mpaka kufanikisha zoezi la kumdhibiti mamba huyo na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli zao Katika ziwa hilo pamoja na kuzingatia elimu inayotolewa na watalamu hao huku akiwahakikishia kuwa Serikali imetenga fedha Kwa ajili ya kuongeza vizimba viwili katika halmashauri ya Buchosa ili kupunguza changamoto ya wanyamapori hao.
Na. Beatus Maganja- TAWA
0 Maoni