Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil
Abdallah ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) kutekeleza maono ya
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia utendaji kazi wenye weledi, ubora na viwango
ili kupata matokeo chanya katika sekta ya biashara nchini.
Ameyasema hayo kwa waandishi wa habari Oktoba 3, 2024 Kibaha
mkoani Pwani baada ya kufungua rasmi kikao cha Menejimenti ya WMA, kukabidhi
magari ili kuboresha utendaji kazi na kuzindua Jarida maalum la Wakala lenye
lengo la kupanua wigo wa uelimishaji na uhabarishaji umma kuhusu WMA.
“Lengo kubwa la kikao chetu ni kukumbushana wajibu na
dhamira nzima ya majukumu yetu ambayo yanatakiwa yaakisi maelekezo na miongozo
ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kuwezesha ufanyaji biashara
ndani ya nchi yetu.”
Ili kuhakikisha maono hayo ya Rais yanafikiwa, Dkt. Abdallah
ameitaka WMA kuzingatia mambo kadhaa ambayo ni pamoja na utii wa sheria,
miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo kwa kuongeza uadilifu na weledi kazini.
Pia, amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja na
kuwa na kauli moja baina ya Bodi, Mkuu wa Wakala, Menejimenti, Viongozi wa
Mikoa pamoja na wafanyakazi wote kwa lengo la kupata matokeo chanya katika
kazi.
Vilevile ameielekeza Menejimenti kuondoa urasimu wa aina
yoyote katika utendaji kazi huku akisisitiza kwamba Jarida alilozindua pamoja
na kutoa habari mbalimbali za Wakala, litumike kama nyenzo ya utoaji taratibu
mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na wadau wa WMA hususani katika ufanyaji
biashara.
Katibu Mkuu amesisitiza Uongozi wa WMA kuzingatia yaliyomo
katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja, ambao unaelekeza kutoa huduma bora na kwa
wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abdallah amempongeza na
kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya
utendaji kazi kwa sekta mbalimbali za umma na kwa muktadha huo kwa WMA ambapo
ametoa jumla ya magari 10 kwa Wakala hiyo ili kuboresha utendaji kazi.
“Leo nimekabidhi magari mawili kwa WMA na mengine Nane yako
kwenye mchakato na tutayakabidhi mara moja utakapokamilika. Kwa hili, tuendelee
kumshukuru sana Mheshimiwa Rais,” amefafanua.
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti nzima, Afisa Mtendaji
Mkuu wa WMA, Alban Kihulla amesema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na
Katibu Mkuu.
Akidadavua kuhusu majukumu ya WMA ambayo ndiyo haswa
yaliyotolewa maelekezo kuongeza nguvu, Kihulla amesema ni pamoja na uhakiki wa
vipimo, ukaguzi wa vipimo pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa kwa lengo
la kukuza uchumi katika sekta mbalimbali.
“Lengo ni kukuza uchumi katika sekta mbalimbali lakini pia
kusaidia wananchi wanaonunua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na
zinazotoka nje ya nchi, ziwe katika uzito sahihi, ujazo sahihi, urefu sahihi
pamoja na namba yaani idadi sahihi.”
Kuhusu magari waliyopokea, Mtendaji Mkuu ameishukuru Wizara
na kukiri kuwa yatapunguza changamoto iliyopo lakini akaomba Wakala iendelee
kufikiriwa kupatiwa mengine zaidi pamoja na vitendea kazi vingine mbalimbali
ili kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi.
Kikao hicho cha Menejimenti ya Wakala wa Vipimo ni utaratibu wa kawaida ambao Wakala umejiwekea ambapo hukutana kila robo ya Mwaka wa Fedha kujadili kuhusu maendeleo ya utendaji kazi na namna ya kuboresha zaidi. Kikao kiliketi kuanzia Oktoba 2, 2024 na kudumu kwa siku tatu ambapo kimejumuisha Menejimenti Kuu kutoka Makao Makuu pamoja na Mameneja wa Mikoa yote Tanzania Bara.
Veronica Simba- WMA, Pwani
0 Maoni