Wakuu wa Hifadhi nchini wametakiwa kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi kwa lengo la kuendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii sambamba na kuimarisha mahusiano mazuri baina yao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb)
amesema hayo jana Oktoba 4, 2024 Mkoani Tabora
alipofanya kikao na Wahifadhi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Maliasili na Utalii wakiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na Chuo cha Mafunzo
ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI).
“Wakuu wa hifadhi muonane na wanakijiji muongee nao ili
muwape elimu ya uhifadhi na muwashauri wawe na Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya
Wanyamapori (WMA) kwenye mapori yetu ya TAWA, TANAPA na TFS,” amesema Mhe.
Chana.
Aidha, amewataka wahifadhi hao kuhakikisha wanaweka alama
zinazoonekana katika hifadhi ili kuimarisha mipaka kwa kushirikisha Serikali za
vijiji vinavyozunguka maeneo hayo.
Ameendelea kusisitiza ushirikiano kati ya taasisi hizo na taasisi zingine za kitaifa na kimataifa kwa kufanya kazi kwa pamoja katika masuala mbalimbali ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uhalifu kwenye maeneo ya hifadhi.
Na. Happiness Shayo-Tabora
0 Maoni