Wakala ya Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro, imetekeleza agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kujenga daraja
la mawe la Lebenya lenye urefu wa mita 45 linalounganisha Wilaya za Kilindi,
Gairo na Kilosa mkoani Morogoro kutoka kwenye fedha zilizobaki wakati wa ujenzi
wa daraja la Berega.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Ikulu (Kazi Maalum), Mhe. Kapt. George Mkuchika alipofika katika daraja
hilo ili kukagua hatua iliyofikia ambapo ujenzi wa daraja hilo umefikia 75%
kukamilika.
Mhe. Mkuchika amesema Mhe. Rais Samia
ametoa mabilioni ya fedha ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi kwa kujenga
upya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana ambazo ziliathiri
miundombinu ya barabara katika maeneo mengi nchini.
"Nimefurahi agizo la Rais Samia
limetekelezwa, hapa mnajengewa daraja tena mawe tupu, daraja hili
litakapokamilika litasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa
hapa," alisema.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA
Wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala alisema wametekeleza agizo la Mhe. Rais
kwamba, kiasi cha fedha shilingi bilioni 1.3 zilizobaki kwenye ujenzi wa daraja
la Berega zitumike kuboresha barabara ya Berega - Kinyolisi - Makuyu Km 18,
ujenzi wa daraja la mawe na maboksi kalavati ambapo mpaka sasa ujenzi wa daraja
umefikia 75% kukamilika na unatarajiwa kukakamilika tarehe 15/05/2025.
Alisema daraja hilo linagharimu
shilingi milioni 373 ambapo kukamilika kwake litanufaisha kata saba zenye jumla
ya wakazi 766,507 na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kwa wakazi wa
wilaya ya Gairo, Kilosa na Kilindi.
“Barabara hii ni njia fupi kutoka
Kilindi mkoani Tanga kwenda Morogoro ambapo ni Km 18 tu kufika njiapanda ya
kwenda Morogoro badala ya kupitia njia ya Gairo ambayo ni Km 44 ambapo
ikikamilika itakuza uchumi kwani wananchi watasafirisha mazao yao misimu yote.”
Naye, mkazi wa kijiji cha
Italagwe-Gairo, Bw. John Semwenda ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja
hilo ambapo alisema litakapokamilika watasafirisha mazao yao hususan mbaazi
kwenda sokoni kwa urahisi.
0 Maoni