Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
imewataka waandishi wa habari kutumia vyombo vyao kuihamasisha jamii kufanya
uchunguzi wa afya zao kwa upande wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya
moyo.
Wito huo umetolewa jana Jijini Dar es
Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali
ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alipokuwa akiongea na wahariri wa vyombo vya
habari waliofika kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika Kliniki ya JKCI
iliyopo Kawe.
“Bado kuna elimu dogo mno kuhusiana na
magonjwa yasiyoambukiza nchini hususan kwa magonjwa ya moyo…na hali hiyo si kwa
Tanzania pekee hadi katika mataifa yaliyoendelea elimu bado ni ndogo,” alisema
Dkt. Shemu.
Amesema kwamba kutokana na hali hiyo
wagonjwa wengi wanafika kupata matibabu wakiwa katika hali ambayo sio nzuri,
ambayo ingeweza kuzuilika iwapo wangepima afya ya moyo mapema.
“Unapopata maumivu makali ya kifuani
upande wa kushoto usipoteze muda kwenda hospitali zingine, haraka sana kimbilia
JKCI ili upate matibabu ya haraka kubaini tatizo, kwani kama ni tatizo la moyo
mtu anaweza kupoteza maisha muda mchache,” alisema Dkt. Shemu.
Magonjwa ya moyo huja kwakushtukiza,
zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaopata mstuko wa moyo hupoteza maisha kutokana
na kuchelewa kupata huduma za matibabu kwa wakati, alisema Dkt. Shemu.
Ameeleza kuwa “Wenzetu wa mataifa
yaliyoendelea wamejitahidi katika kuhakikisha mgonjwa wa moyo anachukuliwa
haraka kwa helkopta na kukimbizwa hospitali ambapo majengo yao hospitali zao juu
yanasehemu ya kutulia.”
Amesema matatizo ya moyo yanapochelewa
kupatiwa tiba katika hatua za awali, tatizo linaongezeka na kuwa kubwa ambapo
pia huchangia kuongeza gharama kubwa za matibabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile ameipongeza JKCI kwa kuwa na maono
ya kuwafikia watu wa aina mbalimbali kuwafanyia uchunguzi wa afya bure kwani bila
hamasa kama hizo wapo watu ambao hasingemudu kupima.
Balile ameeleza kwamba katika zoezi
hilo la kupitia upimaji wa afya ya moyo lililoanza jana na kukamilika leo wahariri
zaidi ya 50 wamejitokeza kwa ajili ya kuangalia afya zao.
Balile pia, ameipongeza Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete kwa huduma bora wanazozitoa katika Kliniki ya JKCI Kawe
iliyopo jengo la Mkapa Health Plaza, ambayo madhari yake ni mazuri na yenye
kumvutia mgonjwa.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakiongozwa
na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Peter Kisenge wamekuwa wakitoa huduma za tiba mkoba
zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya
upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam
na mikoa ya jirani.
0 Maoni