Dereva wa basi la Asante Rabi Shedrack
Swai (37) aliyesababisha ajali iliyoua watu tisa Oktoba 22.2024 eneo la
Ukiligulu, wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza amepandishwa kizimbani jana Oktoba
29,2025 katika Mahakama ya wilaya ya Misungwi na kusomewa shtaka la kuendesha
gari kwa uzembe katika barabara ya umma lenye makosa 64 yakiwemo ya kusababisha
vifo, majeruhi, uharibifu wa miundombinu na mali.
Akisoma shtaka katika kesi ya Trafiki
namba 30855/2024, linalomkabili dereva huyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Esther Marick, Mwendesha Mashtaka wa Serikali,
Ramson Salehe akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lilian Meli amesema
mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27
(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.
Salehe aliieleza Mahakama hiyo kuwa
mshakiwa anashtakiwa kwa makosa 64 yakiwemo ya kuendesha gari kwa uzembe katika
barabara ya umma na kusababisha vifo vya
watu tisa, kujeruhi watu 54 na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na
miundombinu.
“Mshtakiwa (Shedrack Swai) siku ya
Oktoba 22, 2024, ukiwa dereva wa gari lenye namba za usajiri T.458 DYD aina ya
Yutong basi uliendesha gari hilo kwa uzembe katika barabara ya umma
Mwanza-Shinyanga eneo la Kijiji cha Ukiriguru wilayani Misungwi ambapo ulilipita
gari lingine bila kuchukua tahadhari na matokeo yake ukaligonga gari lingine
lenye namba za usajiri T. 281 EFG aina ya You tong basi a kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa
mali,” alisema Mwendesha Mashtaka Salehe.
Baada ya kumsomea makosa hayo,
mshtakiwa Shedrack Swai alikiri kutenda makosa hayo yote 64 huku Wakili wa
Serikali Mwandamizi Lilian Meli akiiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa
ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi
Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Esther Marick alimweleza mshtakiwa kuwa
shtaka linalomkabili linadhaminika na hivyo kumtaka kuwa na wadhamini wawili
wenye barua za utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa, Kitambulisho cha Taifa
(Nida) na bondi ya maneno ya Sh5 milioni kila mmoja.
Hata hivyo mshtakiwa alishindwa
kukidhi masharti ya dhamana baada ya mdhamini mmoja kukosa kitambulisho halisi
cha Taifa cha NIDA hivyo mshtakiwa kupelekwa rumande katika Gereza la Butimba
jijini Mwanza hadi masharti hayo yatakapotimizwa.
Hakimu, Esther aliahirisha shauri hilo
hadi Novemba 5, 2024 litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali.
Mshtakiwa alikamatwa na Jeshi la
Polisi muda mfupi baada ya kusababisha ajali na taarifa ya kukamatwa kwake
ilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP)
Wilbrod Mutafugwa baada ya kukagua eneo la ajali Oktoba 22, 2024. Hata hivyo pia
mstakiwa amefungiwa leseni yake ya udereva na kuondolewa madaraja yake yote.
0 Maoni