Furaha ni kupokezana inaweza kuwa kwa watu wa jamii mbili tofauti kwa wakati mmoja, wakati maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Katavi pamoja na wadau wa uhifadhi na utalii wakisherehekea kilele cha miaka 50 zilienda sanjari na vifijo na ndelemo za wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Sitalike baada ya kukabidhiwa bweni lao lililozinduliwa leo katika hafla ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Sitalike - Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Wakiwa na furaha na bashasha ya kuanza
kutumia bweni hilo, wanafunzi hao walisema, Bweni hilo litapunguza utoro na
visababishi vya mimba vinavyotokana na vishawishi vya barabarani wakati wa
kwenda na kutoka shule.
Akikata utepe jana kuashiria uzinduzi
wa bweni hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliwahasa wanafunzi kutumia nafasi hiyo kushirikiana
kusoma kwa bidii tofauti na awali kila mwanafunzi alikuwa nyumbani kwao.
“Lengo la mabweni ni kuwaunganisha
pamoja ili msome kwa kushirikiana, na mnapomuona mwenzenu analegalega msisite
kumuhamasisha ili aendane na kasi yenu, TANAPA na TEA inawajali ili mtimize
malengo yenu na baadae muwasaidie wazazi wenu,” alisema Mhe. Buswelu.
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi -
TANAPA na Mkuu wa Kanda ya Kusini Steria Ndaga kwa niaba ya Kamishna wa
Uhifadhi - TANAPA aliwataka wanafunzi hao kulitunza bweni hilo ili litumike kwa
muda mrefu, huku pia akiwaonya kutotumia vifaa vinavyoweza kusababisha moto.
Moto husababisha hasara kubwa kwa wanafunzi, kwa shule na taifa kwa ujumla.
Akisoma ripoti ya mradi huo wa bweni
Mkuu wa Shule ya Sekondari Sitalike Samson Kaitira Mafwolo alisema, “Mradi huo
umegharimu kiasi cha shilingi milioni 190 ambapo TANAPA ilichangia zaidi ya
milioni 77, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilichangia zaidi ya milioni 97 na
DED Wilaya ya Nsimbo akichangia milioni 15.”
Kulingana na adha waliokuwa wakipata
wanafunzi hao, Aneth J. Marko kutoka Kidato cha nne alisema, “Bweni hilo licha
ya kutuepusha na vishawishi vya barabarani, pia litatukinga dhidi ya
wanyamapori wakali kwani sehemu kubwa ya makazi yetu yamezungukwa na hifadhi
hii.”
Sherehe hizo za Miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Katavi licha ya uzinduzi wa bweni hilo pia ziliambatana na uzinduzi wa ujenzi wa nyumba 12 za watumishi wa hifadhi chini ya ufadhili wa benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), burudani mbalimbali, na ukataji wa keki kuashiria mwanzo mpya wa hifadhi hiyo huku ikihitimishwa na ziara ya viongozi na wageni waalikwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha na kujione shughuli za uhifadhi, utalii na maeneo ya iwekezaji.
Muonekano kwa ndani wa bweni la wasichana la wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Sitalike lililo kukabidhiwa baada ya kuzinduliwa katika hafla ya maadhimisho hayo yaliyofanyika Sitalike - Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Na. Jacob Kasiri- Sitalike
0 Maoni