Jamii imeshauriwa kuwafikisha hospitalini mapema wagonjwa
wenye changamoto za kiharusi ili waweze kupatiwa tiba sahihi kwa wakati kwa
lengo la kuepuka madhara zaidi yanayoweza kujitokeza endapo mgonjwa huyo
atachelewa kufikishwa hospitalini.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali
ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dkt. Julieth Magandi alipokuwa akitoa elimu kwa
wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kiharusi duniani
yaliyofanyika MNH-Mloganzila.
Dkt. Magandi ameeleza kuwa tatizo la kiharusi ni kubwa na
kuongeza kuwa kwa MNH-Mloganzila katika kliniki ya ubongo na mishipa ya fahamu
kwa siku wanaona wagonjwa kati ya 140 hadi 170 ambapo kati ya wagonjwa hao
asilimia 60 wanabainika kuwa na kiharusi.
“Baada ya kuona
ukubwa wa tatizo la kiharusi Muhimbili Mloganzila tumeamua kuboresha huduma za
magonjwa ya kiharusi kwa kuanzisha kitengo maalum cha kuhudumia wagonjwa wenye
kiharusi ambapo tumeweka vifaa tiba vya kisasa vyenye uwezo wa kufuatilia
mwenendo wa mgonjwa kwa wale wagonjwa ambao wamelazwa wodini.”
Kwa Upande wake Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ubongo
na Mishipa ya Fahamu MNH-Mloganzila Dkt. Mohamed Mnacho amesema kuwa ugonjwa wa
kiharusi ni moja kati ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo na ulemavu
duniani.
Pamoja na hayo, amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO) zinaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 12 duniani wanatatizo la kiharusi
ambapo kati ya hao watu milioni 6 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo kwa
mwaka.
Pamoja na hayo ameitaka jamii kuacha baadhi ya tabia ambazo
zinaweza kuchangia watu kupata ugonjwa wa kiharusi ikiwemo uvutaji wa sigara,
unywaji wa pombe kupita kiasi, uzito mkubwa pamoja kutokufanya mazoezi.
Siku ya kiharusi Duniani huadhimishwa Oktoba 29 kila mwaka ambapo kwa Muhimbili Mloganzila imeadhimisha siku hiyo kwa kutoa huduma mbalimbali bure ikiwemo upimaji wa shinikizo la damu, elimu ya lishe pamoja na ugonjwa wa kiharusi.
0 Maoni