WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
kuwa Serikali inaendelea kutekeleza wa Mpango mkakati wa miaka mitano 2024/25- 2029/30 wa Anga za juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.
Amesema kuwa Taasisi ya Teknolojia Dar
es Salaam imepata mradi wa Utafiti wa kuwezesha urushaji wa satelaiti
unaosimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu
ikishirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JAXA).
Amesema hayo leo (Alhamisi Oktoba 17,
2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Kongamano
la Nane la Mwaka la TEHAMA, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Katika eneo hili Maandalizi ya utungwaji
wa Sera, Sheria na uridhiwaji wa mikataba ya Kimataifa ya masuala ya anga za
juu inaendelea.”
Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwakusanye vijana wabunifu wenye
uwezo wa kubuni teknolojia zenye manufaa kwa Taifa “Lakini simamieni hizi
tafiti zenye kutoa matokeo na vijana hao waendelee kupewa fursa na kazi hizo
ziingie kwa jamii na zianze kutumika.”
Pia Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza
Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari isimamie na kuhakikisha
ujenzi wa Vituo vya Ubunifu (Innovation Hubs) katika mikoa iliyokubalika
unafanyika kama ilivyopangwa.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa mabadiliko ya kidijitali ni lazima na Safari hiyo haipaswi kumuacha mtu
yeyote nyuma hususan kwenye mfumo wa kifedha jumuishi. “Kama mnakumbuka,
Serikali katika mwaka 2020 ilizindua Mfumo wa N-Card ambao hadi kufikia sasa
umefanikiwa kuwaunganisha wananchi wasiopungua milioni nne. Mfumo huo umesaidia
sana kuokoa upotevu wa fedha katika vituo vya usafirishaji”
Ameongeza kuwa mfumo huo umesaidia
kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato. “Nitoe wito kwa Wizara kuhakikisha
maeneo mengi ambayo Serikali imewekeza yanatumia mfumo wa N-card. Mfumo huo ni
muhimu katika kuokoa upotevu wa fedha za Serikali na kuwasaidia wananchi kuacha
kutembea na fedha taslimu na watumiefedha kwa njia ya kidijitali.”
Katika hatua nyingine Mheshimiwa
Majaliwa ameitaka Wizara ya Mawasiliano, Habari na Teknolojia ya Habari
ihamasishe matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma, biashara na uzalishaji ili
kuongeza uwazi, ufanisi na kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii;
Kwa Upande wake Waziri Habari,
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema kuwa Serikali
imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambapo kwa
mwaka fedha 2023/24 jumla ya urefu wa kilomita 1,592 za mkongo wa taifa
zimejengwa na kufika katika wilaya 83.
“Pia umoja wa watoa huduma za
mawasiliano (consortium of telecom operators) wameweza kujenga jumla ya
kilomita 2,595 ambazo zinafanya mkongo wa taifa kuwa na kilomita 13,820. Wizara
imehamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mkongo wa taifa wa
mawasiliano na kituo cha kuhifadhia data (NIDC) kwenda katika Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL).”
Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) Bi. Nardos Bekele-Thomas amempongeza
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha
Tanzania inatumia ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika kuchagiza Maendeleo Endelevu
nchini.
0 Maoni