Matumizi ya pombe yaliyopitiliza yanaweza kusababisha magonjwa ya mishipa ya fahamu

 

Matumizi ya pombe yaliyopitiliza yanaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa fahamu kwa kuwa kemikali zilizopo kwenye pombe zina tabia ya kuleta madhara kwenye seli za mfumo wa balansi ya ubongo ambapo mwisho wake seli za ubongo zinaweza kufa kabisa.

Kauli hiyo imetolewa na Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu MNH-Mloganzila, Dkt. Mohamed Mnacho na kuongeza kuwa mtu akinywa pombe na kulewa maana yake anakuwa ameathiri mfumo wa balansi ya ubongo hivyo akiendelea na tabia hiyo mara kwa mara seli za ubongo zitakufa.

Dkt. Mnacho amebainisha kuwa mtu aliyeathirika na changamoto za mfumo wa balansi za mfumo wa ubongo ataanza kupata changamoto za kusahau, kutetemeka, kuchanganyikiwa na baadaye anaweza kupata kifafa ambacho kitampelekea kutumia dawa za kifafa kila siku.

“Ni vizuri jamii ikajiepusha na matumizi ya pombe yaliyokithiri kwa kuwa pombe ikizidi inakuwa ni sumu na madhara yake ni ya muda mrefu na mtu akipata magonjwa haya yatokayo na athari ya matumizi ya pombe matibabu yake yana gharama kubwa na yanatumia muda mrefu kuyatibu,” ameongeza Dkt. Mnacho.

Ni vema kama mtu anahitaji kunywa pombe akatumia si zaidi ya chupa moja ili kuendelea kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu.

Chapisha Maoni

0 Maoni