Imeelezwa kwamba Wizara ya Madini
kupitia Mpango wa Uchimbaji Madini wa Kesho yenye matumaini (MBT) kwa vijana
watakaohitimu katika Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) kuwawezesha kwa
kuwapatia vifaa na mashine za Uchongaji, Ukataji na Usafishaji madini ghafi
zitakazo pelekea kuwa bidhaa bora zenye thamani ya juu.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 16, 2024 na
Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja
zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema kuwa, Kituo cha
TGC kinatoa mafunzo kupitia vifaa vya
kisasa hususan katika uongezaji thamani madini ya vito kwa Ukataji Uchongaji na
Usafishaji, hivyo kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 wizara kupitia TGC chini ya
Mpango wa MBT itawapatia vifaa na
mashine za kisasa kwa wahitimu
watakaomaliza masomo ili waweze kujiendeleza baada ya masomo kumalizika.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa, lengo
la wizara ni kuwa na KanziData inayoonesha maendeleo ya wahitimu katika
kuendeleza ujuzi wa kiufundi na ubunifu walioupata na kuutumia katika viwanda
vya kuongeza thamani madini nchini.
Sambamba na hapo, Waziri Mavunde
amesisitiza kuwa Mpango mwingine ni kuwepo kwa madini mengi ya vito yaliyoongezewa
thamani katika ubora mzuri wa muonekano, ukataji, rangi na uzito ambayo
yatawekwa katika vituo vya biashara ili kutanua masoko ya ndani ya nchi.
Kwa upande wake , Naibu Waziri wa
Madini Dkt.Steven Kiruswa ameeleza kwamba , faida za Mpango wa MBT kwa wahitimu wa TGC ni pamoja na kuwapatia
fursa za masoko, kupata ujuzi wa kisasa kupitia vifaa, kukuza ujasiriamali na
Kuchangia Maendeleo ya Sekta ya Madini kwa kuongeza thamani madini kabla ya
kusafirisha nje ya nchi.
Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu
Utendaji Kazi wa Kituo cha TGC , Kaimu Mkuu wa Kituo Mhandisi Ally Maganga
amesema kuwa, katika kipindi cha Oktoba 2023 mpaka Septemba 2024 jumla ya vipande vya madini ya vito 395 yenye
jumla ya uzito wa carat 335.43 yalikatwa.
Aidha, jumla ya bidhaa 78 za urembo
zilitengenezwa kwa kutumia metali za thamani ikiwemo dhahabu na fedha ambapo
vinyago vya thamani madini 541 vilitengenezwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti ,
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe.Kilumbe Ng'enda ameipongeza Wizara ya
Madini na taasisi zake kwa kuratibu na kusimamia mipango mbalimbali inayopangwa
ndani ya wizara kwa lengo la utekelezaji na kutoa matokeo chanya kwa sekta na
taifa kwa ujumla.
Kituo cha TGC kilianzishwa Mwaka 2003,
kabla ya hapo kituo kilijulikana kama Arusha Gemstone Carving Center (AGCC).
0 Maoni