Kutokana na chanjo kutajwa kuwa na
umuhimu mkubwa kwa Kinga ya watoto ikiwemo kuzuia uwezekano wa ulemavu wa
kuona, Mstahiki Meya Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora Mhe. Ramadhan Kapera
amesema Manispaa hiyo itakuja na Operesheni maalum ya kuhamasisha jamii umuhimu
wa kuwapeleka watoto kupata chanjo.
Akizungumza Mjini Tabora katika
Ufunguzi wa Mafunzo ya namna bora ya kutatua changamoto ya Huduma za chanjo
kwenye jamii kwa kutumia bunifu mbalimbali (Human Centred Design-HCD) Mhe. Kapera
amesema suala la chanjo ni lazima liwe katika ajenda ya Manispaa.
"Katika kulibeba hili jambo liwe ajenda katika
Manispaa tumekubali kama maagizo na tutahakikisha tunaweka Operesheni maalumu
kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa chanjo,"amesema.
Aidha, Mhe. Kapera amesema katika
kufanikisha jambo hilo ni lazima watumishi kutoka Manispaa hiyo hasa kupitia
Sekta ya Afya kwenda kwenye jamii kutoa elimu ya Afya kuhusu umuhimu wa chanjo.
"Ili kufanikisha hili ni lazima
wananchi wapate elimu na wasijifungie ndani, jukumu letu kama viongozi ni
kwenda mitaani, hili jambo linatakiwa lijulikane kwa Wananchi kama uchaguzi na
hakuna mwananchi ambaye hajui sasa Kuna uchanguzi wa Serikali za Mitaa kwani
katika kukinga Magonjwa haya ya watoto wanatakiwa wapewe chanjo,
"amesisitiza.
Kwa upande wake Simon Nzilibili kutoka
Wizara ya Afya,Idara ya Kinga, Sehemu ya
Elimu ya Afya kwa Umma amesema suala la ushirikishaji kwa Jamii una mchango
mkubwa katika kusaidia kutengeneza mikakati ya
kuimarisha ya mwitikio wa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka
mitano ili kuimarisha Kinga huku akitoa
wito kwa jamii kuendelea kuwa na mwitikio wa kuwapatia watoto chanjo.
"Ni muhimu kushirikisha Jamii
katika kuleta msukumo wa mwitikio wa chanjo na nitoe wito kwa jamii hasa wazazi
na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 wanapata chanjo,"
amesema.
Enock Mhehe ni Afisa Mpango kutoka Wizara ya Afya, Mpango
wa Taifa wa Chanjo amesema wamelenga
katika makundi mbalimbali ya kijamii kutoa Mafunzo ya umuhimu wa chanjo ikiwemo
Waandishi wa Habari, Makundi ya watu wenye ulemavu, Viongozi wa dini,
wafanyabiashara wadogo huku akizungumzia umuhimu wa chanjo ikiwemo kinga kwa
watoto wadogo.
"Magonjwa yanayozuilika kwa
chanjo hayana tiba, na tiba yake ni chanjo na chanjo za watoto zipo za aina
nyingi ikiwemo kuhara ,kifua Kikuu, Pepopunda, Kifaduro, Surua na Rubella,"
amesema.
Mganga Mkuu Manispaa ya Tabora Dkt.
Shani Mudamu amesema wamelenga kufikia makundi yote ya watoto kupata chanjo.
"Hadi kufikia mwezi Septemba
mwaka huu hatukufikia malengo ya asilimia 90% kwa watoto walio na umri chini ya
miaka 5 hivyo kupitia haya Mafunzo tunatakiwa tuibue changamoto zinazokwamisha,"
amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona
Manispaa ya Tabora Ahmmad Issa ametumia
fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo na atakuwa balozi kwa
wengine huku akizungumzia namna alivyopata ulemavu wa macho wa kudumu(upofu)
baada ya kukosa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua akiwa na umri wa miaka
miwili.
"Nashukuru Serikali kwa kuona
umuhimu wa jambo hili la Mafunzo, kilichosababisha mimi niwe kipofu ni kukosa
elimu ya Afya kuhusu matumizi sahihi ya
chanjo kwa wazazi wangu, Jamii inapokosa matumizi sahihi ya chanjo, ndio
matokeo yake kama nilivyo, hivyo ni muhimu tuondoe mila potofu dhidi ya chanjo, lengo letu tuwe na jamii
iliyokamilika," amesisitiza.
Ikumbukwe kuwa Mafunzo ya "Human
Centred Design-HCD" yanalenga kuimarisha hamasa ya Huduma za Chanjo kwa
watoto hasa kwa kushirikisha Jamii namna ya kutatua changoto zinazokwamisha
suala la chanjo.
Na. Faustine Gimu- Wizara ya Afya, Elimu ya Afya kwa Umma
0 Maoni