WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wahakikishe wanalinda utamaduni na kujenga misingi ya kuhamasisha vijana na vizazi vijavyo kutambua na kuenzi historia na urithi wa Mtanzania.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila
Mtanzania kutunza utamaduni, mila na desturi kwa sababu utamaduni ni nguzo ya
utambulisho wa jamii husika na ni muhimu kwa kizazi kijacho.
Amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 27,
2024) wakati akifungua Tamasha la Buhaya 2024 ‘Buhaya Festival’ lililofanyika
katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Katika siku za sasa, ambapo
teknolojia na utandawazi vinazidi kuimarika, ni rahisi kupoteza mila na desturi
zetu, hivyo tunaposhiriki tamasha hili, tunajifunza na kuhamasisha jamii zetu
kuhusu umuhimu wa urithi wetu wa kiutamaduni.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa
amewaasa wazazi, jamii na madhehebu ya dini kuendelea kuhimiza utunzaji wa
maadili kwa kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa
vijana na jamii kwa ujumla.
“Watanzania wote tuendelee kuheshimu
na kuenzi tamaduni zilizo nzuri kama njia ya kuimarisha umoja, mshikamano na
maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa
Majaliwa ameagiza Mikoa yote nchini kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya
kiserikali na sekta binafsi iweke mipango ya kuandaa matamasha ya utamaduni
kuanzia ngazi za Wilaya ili kuendeleza na kuhifadhi vivutio, mila na desturi za
maeneo husika.
Akizungumzia kuhusu Maendeleo ya Mkoa
wa Kagera, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo katika mkoa huo kwenye sekta za nishati, maji, kilimo, uvuvi, uchukuzi
na ujenzi wa barabara.
0 Maoni