Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith
Kapinga amesema Serikali inatarajia kuanza mradi mpya wa upelekaji umeme kwenye vitongoji utakaohusisha ujenzi wa njia za kati na ndogo za kusafirisha umeme.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Oktoba
31, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. George
Mwanisongole, Mbunge wa Mbozi aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza
kupeleka umeme mkubwa kwenye vitongoji ambavyo havijapata umeme mkubwa na hivyo
kukosa sifa ya kuwepo kwenye miradi ya maendeleo.
"Kwenye mradi huu utakaoanza
Desemba 2024 tumeboresha zaidi kwani tutakuwa na transfoma zenye ukubwa wa KVA
50, 100 na 200 kulingana na ukubwa wa Kitongoji," amesema Mhe. Kapinga.
Ameongeza kuwa, maeneo ya vitongoji
ambayo hayakunufaika na mradi wa awali wa vitongoji 15 yatanufaika kwa mradi
utakaoanza Desemba 2024.
Akijibu swali la Mbunge wa Iringa
Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu aliyeuliza ni lini Serikali itatekeleza ahadi
ya umeme jazilishi maeneo ya Miji yenye sura za Vijiji kama Ugele, Mosi,
Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina, Mhe. Kapinga amesema
Serikali inaendelea kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini yakiwemo maeneo ya miji yenye sura za vijiji.
Aidha, kwa maeneo ya Ugele, Mosi,
Cargrielo, Machinjio, Ulonge, Mtalagala na Msisina yaliyopo katika Jimbo la
Iringa Mjini, Serikali itayapelekea umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme
katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo.
Ameongeza kuwa, maeneo ya Cargrielo na
Machinjio yatapatiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia miradi yake ya ndani ya kusogeza
miundombinu ya umeme kwa wananchi.
0 Maoni