Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Wakili
Mariam Msengi amewataka wananchi wilayani humo kuzingatia lishe bora katika
ulaji wao wa kila siku huku akisisitiza umuhimu wa taifa kuwa na wananchi wenye
afya nzuri katika kuijenga nchi.
Akizungumza wakati wa kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Lishe katika Mtaa wa Nyambiti uliopo kata ya Buzuruga
wakili Msengi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka juhudi kubwa
katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma bora za afya kwa
kuimarisha miundombinu mbalimbali ya sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
vituo vya kutolea huduma hizo ndani ya Manispaa hiyo huku mkazo wa utoaji elimu
ya lishe ukiendelea.
"Kina mama sisi ndo viongozi wa
familia katika mambo haya, tuwe mstari wa mbele kuzingatia lishe bora kwa
familia zetu," Wakili Msengi.
Akitoa taarifa wakati wa maadhimisho
hayo Afisa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khasim amesema takwimu za mwaka
2023/2024 zinaonyesha asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano
wamedumaa, asilimia 12 wana uzito pungufu na asilimia 3 wana ukondefu sambamba
na hali duni kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (mwaka 15 - 49).
"Tunayo mafanikio tangu
kuanzishwa kwa mpango wa lishe kitaifa ikiwemo kuongezeka kwa mwitikio wa jamii
kuhudhuria elimu za lishe na kuleta watoto kupata nyongeza ya matone ya vitamin
A na dawa za minyoo ambapo lengo lilikuwa watoto 66,381 na tukapata watoto
66,711 sawa na asilimia 100.4.”
Naye Diwani wa kata ya Buzuruga Mhe. Manusura
Sadick Lusigalie amewataka wananchi wake kuunga mkono serikali ya Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuzingatia ulaji sahihi wa makundi yote muhimu ya vyakula ili
kuleta nguvu kazi yenye matokeo chanya kwa Taifa.
Huduma zilizotolewa wakati wa
maadhimisho hayo ni pamoja na kipimo cha HIV na sukari, chanjo mbalimbali kama
polio,chanjo zote za watoto,matone ya vitamini A na dawa za minyoo na kipimo
cha urefu na uzito wa mwili sambamba na jiko darasa.
0 Maoni