Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Mwalimu ni Nyota inayoangaza na
hivyo kama Taifa tuwaheshimishe walimu wa Tanzania na Kuinua taaluma ya Ualimu
ambayo imekuwa chanzo cha maarifa kwa Watoto wetu pia tuwahimize wailinde kwa
wivu mkubwa taaluma hiyo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza
na Wananchi wa Ushirombo kwenye mkutano uliofanyika katika eneo la Ng’anzo,
Mkoani Geita ambapo amebainisha sababu ya Wilaya ya Bukombe kufanya vizuri
katika sekta ya Elimu ni kutokana nia yake tangu mwaka 2015 wakati anachaguliwa
kuwa Mbunge, Wilaya ilikuwa ikishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya Taifa.
“Nilizungumza na walimu kuhusu matokeo
mabaya na wao wakaniambia tusiwaache nyuma hivyo tulianza kukutana na kufanya
tathimini na sasa tunafanya vizuri,” ameeleza Dkt. Biteko.
Ametaja kupanda kwa viwango vya ufaulu
kila mwaka “Katika matokeo ya mwaka jana darasa la saba mkoa tulikuwa nafasi ya
pili, darasa la nne tulipata wastani wa asilimia 78 na kuwa nafasi ya pili
kimkoa, upande wa Kidato cha pili tulikuwa na ufaulu wa asilimia 98 na mitihani
ya kijipima ya Wilaya ya Bukombe tumeshika nafasi ya tatu hivyo niliona tutenge
siku moja ya kusema asante mwalimu.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Ualimu
ni kazi Takatifu, Kazi hii ilifanywa na Yesu, kazi hii aliifanya Mtume Mohammad
S.W.A, Ni kazi ambayo inamzalisha Daktari, Mzazi, Kiongozi na Mwalimu mwingine
mwelevu hivyo walimu nchini wasivunjike mioyo bali waendelee kufanya kazi yao
yenye kielelezo cha mafanikio katika Taifa na kuwa Walimu ni Nyota inayoangaza
na yeye ataendelea kushirikiana nao.
“Nataka niwaambie walimu wote nchini
Serikali inathamini na kutambua mchango wenu kwa Taifa letu na Rais Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta
ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi yenu na tayari amepandisha vyeo
walimu 1,036," amebainisha Dkt. Biteko.
0 Maoni