Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko tayari kuendelea kushirikiana na viongozi
wa dini kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu maendeleo na ustawi
wa nchi.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba
27, 2024 Jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika ibada maalum ya shukrani ya kuadhimisha miaka 50 ya Pastoreti ya
AICT Magomeni.
“Mhe. Rais anakumbuka namna
mnavyomshirikisha katika masuala
mbalimbali yanayohusu kanisa na kwa kweli milango yake iko wazi
anawakaribisha wakati wowote ili muweze
kutoa maoni yenu ya namna ya tunavyoweza kuiongoza nchi yetu,” amesema Dkt.
Biteko.
Vilevile, Dkt. Biteko amesema
maadhimisho ya jubilee ni kukumbuka wakati uliopita na kuangalia eneo gani
lilifanyiwa kazi vizuri na lipi linahitaji kuboreshwa.
Amewahimiza waumini wa Kanisa hilo
kujitoa kwa hali na mali katika kulijenga Kanisa bila kusubiri kesho “Wito
wangu kwetu tusiangalie leo tuangalie miaka 200 kanisa hili litakuwa wapi,
tusisubiri kesho kwa kuwa hatuijui kesho itakuwaje. Fanya chochote unachoweza
kufanya leo na kazi ya leo kisiwe kikwazo cha kazi ya kesho.” amesema Dkt.
Biteko
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito
kwa Kanisa hilo kuendeleza umoja miongoni mwa waumini wake na Watanzania na
kusema kuwa wafuate misingi ya uanzilishwaji wake ambayo ni kujitawala,
kujiendesha na kujieneza.
“Hubirini upendo na msiruhusu mtu kutugawa wala
kutubagua, Mungu ametupa nchi nzuri yenye rasilimali za kutosha, niwaombe
Maaskofu na wachungaji wa Kanisa hili msivunjike moyo kusudi mliloitiwa na
Mungu lisimamieni na waumini wa Kanisa hili tuwe sauti nzuri tuwasaidie
viongozi wetu na tuwatie moyo,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, amelipongeza Kanisa la AICT kwa kuendelea kutoa hamasa kwa jamii na
kuwakumbusha Watanzania kushiriki uchaguzi huo na kuchagua viongozi wenye sifa.
Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu
Mkuu wa AICT, Musa Magwesela amesema kuwa ibada hiyo ni muhimu kwa kuwa tangu
kuanzishwa kwa Magomeni mwaka 1974 limekuwa na mchango muhimu katika kutangaza
injili.
“Kuna sababu 14 za kuhubiri utukufu na
maajabu ya bwana, Kanisa hili la Magomeni kwa mujibu wa Zaburi ya 96 tumetumia
njia 12 kuhubiri jina la bwana, ikiwemo kutumia nyimbo,” amesema Askofu
Magwesela.
Askofu Magwesela ameongeza kuwa wakristo
wamehimizwa kutenda matendo mema, kutumia vipaji na kutumia karama zao.
Aidha, amesema Kanisa linatambua
michango ya watu mbalimbali waliyotoa wakati wakifanya kazi katika Kanisa hilo
la Magomeni huku akitaja majina ya baadhi ya wachungaji waliohudumia kanisa
hilo“ Wito wangu tuenzi michango ya waliohubiri utukufu na maajabu ya bwana,”
amebainisha Askofu Magwesela.
Vilevile, katika kuunga mkono jitihada
za Rais Mhe. Dkt. Samia, Askofu Magwesela amesema kuwa Oktoba 26, 2024 Kanisa
hilo limegawa mitungi 20 ya nishati safi ya kupikia kwa jamii inayozunguka
Kanisa.
Sambamba na ibada hiyo, Kanisa hilo
limeendesha harambee kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kanisa, ofisi na
madarasa ya watoto, ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amechangia kiasi
cha shilingi milioni 100.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni