Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
kuwa mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la TAKUKURU pekee bali kila Mtanzania
anapaswa kushiriki kikamilifu kusimamia maadili na kupinga vitendo vya rushwa.
Amesema kuwa rushwa inaweza
kusababisha kutofikiwa kwa jukumu la Serikali la kuleta ustawi wa wananchi
linalotamkwa katika Ibara ya 8(1)[b] ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Amesema hayo leo jana Oktoba 26,
2024, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya ufungaji wa
mafunzo ya awali ya uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini
(TAKUKURU), yaliyofanyika kwenye Shule ya Polisi Tanzania, Moshi mkoani
Kilimanjaro.
“Hili ni jukumu la kila Mtanzania na
wadau wote muhimu hapa nchini, rushwa ni adui wa haki na maendeleo katika
jamii, Vitendo vya rushwa rushwa vinasababisha uchepushaji wa rasilimali kutoka
kwenye matumizi sahihi na kuathiri haki za kiraia. Katika utumishi wa umma,
rushwa inavuruga ushindani wenye usawa na inaathiri rasilimaliwatu ya nchi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais
Dkt. Samia anawategemea watumishi wa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa
nchini na kuhakikisha wanaimaliza kabisa vitendo vyote vya rushwa “Ameniambia
niwaambie kuwa hatawaangusha kamwe.”
Amesema kuwa rushwa ni changamoto ya
kidunia ambayo kwa nchi zinazoendelea linachochewa na umaskini uliokithiri,
ujinga na mmomonyoko wa maadili. “Rushwa ni changamoto inayotokana na kuahidi,
kutoa, kupokea au kushawishi moja kwa moja au kupitia wakala, Sisi kama Taifa
eneo hili lazima tulisimamie.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewaeleza wahitimu hao kuwa wanapaswa kwenda mpaka vijijini kuelimisha umma kuhusu athari za rushwa “Kamanda wa TAKUKURU unapaswa kulisisitiza hili, badala ya kukuta watumishi wapo ofisini kuanzia asubuhi mpaka jioni, tunatarajia mpite huko muone na muwasisitize waende field.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza
TAKUKURU iongeze kasi na mikakati ya kudhibiti rushwa hasa katika maeneo ya
ukusanyaji mapato, manunuzi wa umma, michakato ya ajira katika utumishi wa
umma, mifumo ya ugawaji wa ardhi, utoaji wa huduma za jamii. “Pia Endeleeni kuongoza
ufuatiliaji na usimamizi wa karibu wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George
Simbachawene amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa alioufanya
ikiwemo ununuzi wa magari, ujenzi wa majengo katika ofisi za TAKURURU wilaya na
mikoa ajira za maafisa uchunguzi ambao wataongeza nguvu katika mapambano dhidi
ya rushwa nchini.
“Kazi kubwa aliyoifanya Rais Dkt.
Samia inatufanya tukose kisingizio, ni lazima tulipe dhamani ya uwekezaji huu
katika kupambana na rushwa usiku na mchana kwa vitendo na kuhakikisha rushwa
hailitafuni Taifa, Mimi na Wenzangu Wizarani tutahakikisha uwekezaji huu
unaleta tija katika mapambano dhidi ya Rushwa nchini.”
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Crispin Chalamila amemweleza Waziri Mkuu kuwa katika kipindi cha miaka mitatu
ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani, TAKUKURU imepatiwa
jumla ya Shilingi bilioni 30 za kununulia magari 195 ambapo 88 yameshanunuliwa.
“Magari haya mapya 10 uliyokabidhi
ikiwa ni ishara ya kukabidhi magari 88 ni sehemu ya magari hayo, Mchakato wa
kununua magari 107 yaliyobakia unaendelea na tunatarajia kuyapata hivi
karibuni, tunaahidi kutatunza magari haya ili kuongeza tija katika utendaji
wetu,” amesema Bw. Crispin.
Waziri Mkuu amekabidhi magari hayo
wakati anafunga mafunzo ya awali ya uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa Nchini (TAKUKURU), hafla inayofanyika kwenye Shule ya Polisi
Tanzania, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo,
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu TAKUKURU Bw. Ayoub Akida
amesema kuwa jumla ya washiriki waliohitimu mafunzo hayo ni 436, ambapo
wanawake ni 175 na wanaume 261. “Washiriki hawa wamegawanyika katika makundi
mawili ambapo kundi la kwanza ni la Maafisa Uchunguzi 323, wanaume wakiwa ni
182 na wanawake 141, na kundi la pili ni la Wachunguzi Wasaidizi 113, wanaume
wakiwa ni 79 na wanawake ni 34.”
Ameongeza kuwa Lengo la mafunzo hayo
ni kuwaandaa wahitimu hao ambao ni waajiriwa wapya wa TAKUKURU, kutekeleza
majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
0 Maoni