Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewaasa wanajamii kutenda matendo mema ya kuigwa na vizazi vijavyo ili
kuweka historia na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 6, 2024 katika Ibada ya
Kumbukizi ya Askofu wa kwanza wa Kanisa la African Inland Church Tanzania
(AICT), Jeremia Mahali Kisula iliyofanyika Kanisa Kuu (AICT) Makongoro Jijini
Mwanza.
“ Leo Askofu Kisula
ametajwa sana kwa sababu ya maisha yake miaka 40 baada ya kifo chake. Mtu huyu
alifanya kazi ya kutangaza injili katika mazingira yale ambayo leo tunajiuliza
mtu anawezaje kusafiri wakati huo bila uwepo wa miundombinu na vyombo vya
kisasa kama ndege na SGR,” amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua kuwa historia
itamtaja marehemu Askofu Kisula
kama kiongozi wa kwanza wa AICT
na kuwa ni lazima kuendelea kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyofanya katika kanisa
hilo.
“Maisha yetu ni lazima yawe ya kuacha alama ili watakokuja
nyuma yeti wakute tuliyoacha mazuri au mabaya na kwa maisha ya kawaida mtu atachukua
mema na kuepuka mabaya. Viongozi na waumini tujue viongozi wana uwezo
kutuelekeza kwenye jambo au maono fulani na kutufanya tuamini, tuna wajibu
mmoja wa kumuenzi Askofu huyu kwa yale yote aliyotufundisha na hasa
kujitegemea,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa waumini wa AICT wana wajibu wa kuhakikisha
wanaendeleza kanisa na utamaduni wa kujitegemea kwa kutoa michango mbalimbali
inayolenga kuimarisha kanisa.
Sambamba na kupongeza familia kwa kushiriki ibada ya
shukrani huku akiwataka kuendeleza umoja miongoni mwao.
Akizungumzia viongozi wa dini wa AICT, Dkt. Biteko amewaasa
viongozi hao kuendeleza kazi yao ya utumishi bila kujali vikwazo mbalimbali wanavyokumbana
navyo. “ Dunia hii ina sauti mbili ya ndani na nje, isikilizeni sauti ya ndani
na msisikie ya nje ambayo itawavunja moyo, waumini tutaendelea kuwa sauti ya
nje iliyo njema,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Mhe. Dkt. Rais Samia
anaamini kuwa anaiongoza nchi isiyo na dini ila wananchi wake wana dini na kuwa
amewaelekeza viongozi wa Serikali kusikiliza maoni ya viongozi wa dini na
kuifanyia kazi ili mchango wao utumike kujenga nchi na Taifa lenye umoja.
Akihubiri katika ibada hiyo Makamu Askofu Mkuu Zakayo Bugota
amesema kuwa utamaduni wa kushukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya mtu
aliyefariki dunia ni utaratibu mzuri unaostahili kuendelezwa ikiwa ni njia
mojawapo ya kuwaenzi viongozi waliitenda mambo mema wakati uhai wao.
“Unapoishi nini utaachia jamii yako ili ukumbukwe na kuigwa, sio tu kuishi jamii yangu au kanisa langu watapata nini cha kuiga?,” amehoji Makamu Askofu Bugota.
Ametaja sifa mojawapo ya Askofu Kisula kuwa hakutaka Kanisa
la AICT kuwa tegemezi hivyo alitaka lijitegemee kwa kuhimiza waumini wake
kujitoa kwa ajili ya kujenga kanisa hilo.
Makamu Askofu Bugota ameongeza “Askofu Mzee Jeremia Kisula
na sisi tusisitize jambo la imani ya kumfuata Yesu Kristo inapaswa kuwa imani
ya kuigwa na turithishe watoto wetu, na tuonyeshe mfano mzuri wa kumfuata Yesu
bila kubadilika.”
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala amemshukuru Askofu wa
AICT kwa kuendelea kutoa huduma na kushirikiana na Serikali katika masuala
mbalimbali yanayolenga kuleta maendeleo ya wananchi.
Pia, amesema kuwa wakati Watanzania wakielekea kwenye
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 Mwaka huu, wakazi wajitokeze
kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura tarehe 11 hadi 20, mwaka huu ili
kupata kuwachagua viongozi wanaofaa.
Ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi katika tukio la
Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere
ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Naye, mtoto wa marehemu Askofu Jeremia Mahali Kisula, Adella Kisula amesema kuwa shukrani ni neno lenye upendo na neema na kuwa wameshiriki ibada hiyo ikiwa ni ishara ya alama aliyoiacha baba yao.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni