Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameithibitishia Jumuiya ya Kimataifa
kuwa masuala ya demokrasia na haki za binadamu yataendelea kuimarika zaidi
nchini Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Nchimbi aliyasema hayo
alipokutana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Dr. Mehmet Güllüoğlu,
Balozi wa Morocco, Mhe. Zacharia El Goumir, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa
Sera na Tathmini wa Taasisi ya Misaada ya Marekani (MCC), kwa nyakati tofauti, jana
tarehe 15 Oktoba 2024.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, Balozi
Nchimbi amesema katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita, hatua
kubwa imefikiwa katika kuimarisha demokrasia, utawala bora, uchumi na haki za
kiraia.
Mazungumzo hayo ya Balozi Nchimbi na
mabalozi wa nchi hizo, pamoja na taasisi ya MCC, yalilenga kuboresha uhusiano
katika nyanja mbalimbali, zikiwemo siasa, kilimo, teknolojia, elimu, na michezo,
kwa lengo la kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wa pande zote.
Katika kikao chake na Balozi wa
Uturuki Mhe. Dkt. Güllüoğlu, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa uhusiano wa
Tanzania na Uturuki ni wa kimkakati, huku akitaja ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)
kuwa ni mfano mmojawapo wa mafanikio ya ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mhe. Dr. Güllüoğlu
alikubaliana na Balozi Nchimbi na akathibitisha kuwa Uturuki itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, zikiwemo sekta za
teknolojia, elimu na biashara ya mazao ya kilimo.
Katika mazungumzo yake na Balozi wa
Morocco, Balozi Nchimbi aliishukuru nchi hiyo kwa mchango wake katika sekta ya
elimu na michezo na kuipongeza kwa msaada wao wa ujenzi wa msikiti mkubwa
kuliko yote Afrika Mashariki, uliojengwa eneo la Kinondoni jijiji Dar es
Salaam.
Balozi Nchimbi alibainisha kuwa
ushirikiano wa Tanzania na Morocco una manufaa makubwa kwa pande zote mbili,
hasa katika kukuza elimu, michezo, na masuala ya usalama ndani ya Afrika.
Kwa upande wake Balozi wa Morocco Mhe.
Goumir alithibitisha kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku
akieleza dhamira ya Morocco katika kusaidia maendeleo ya kitaaluma na michezo
nchini Tanzania.
Aidha, mazungumzo ya Balozi Nchimbi na
ujumbe wa MCC, uliongozwa na Mhe. Dan Barnes, yalijikita katika maeneo ya
siasa, miradi ya maendeleo na utawala bora.
Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa
Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia, inaendelea kuchukua
hatua madhubuti katika kuboresha hali ya demokrasia na haki za binadamu nchini.
Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa
maendeleo haya ni sehemu ya dira ya serikali ya kuhakikisha kuwa haki za raia
na utawala bora vinadumishwa, huku Tanzania ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa
barani Afrika na dunia kwa ujumla.
0 Maoni