Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Mabula Misungwi Nyanda akiongozana na Maofisa waandamizi wa Taasisi hiyo Oktoba 16, 2024 amekutana na Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Kemori Chachakwa ajili ya kujadili mustakabali wa utatuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo inayowakabili wananchi wilayani humo.
Kamishna Mabula ameeleza namna Taasisi
yake inavyotekeleza jukumu la kupambana na changamoto ya wanyamapori hao ili
kuwaondolea adha wananchi na namna ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa
akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma Septemba, 2024 kuhusu kukabiliana na
changamoto ya wanyamapori hao Katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.
Mabula amesema TAWA inatarajia
kuongeza vitendea Kazi ambapo Katika wilaya ya Tunduru itaongeza gari 1 na
Pikipiki 2 zitakazotumiwa na Askari wahifadhi Kwa ajili ya mwitikio wa haraka
wa matukio ya tembo, ikiwa ni pamoja na mabomu baridi 250 Kwa ajili ya
kuwafukuza wanyamapori hao kutoka katika makazi ya watu.
Ili kuimarisha utendaji kazi, Kamishna
Mabula amesema TAWA imejenga kituo cha Askari wa kudumu eneo la Chingulungulu
na hivi karibuni itaongeza idadi ya
Askari wahifadhi wapatao 20 Katika kituo kidogo cha Songea ili kuwaongezea nguvu
Askari 8 waliopo sasa wilayani Tunduru ikienda sambamba na kuanzisha kituo cha
muda cha Askari katika tarafa ya Namasakata.
Katika hatua nyingine Kamishna Mabula ametumia ziara hiyo kuongea na Maafisa na Askari wa uhifadhi ili kusikiliza changamoto wanazopitia Katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhimiza utendaji Kazi unaozingatia Sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kusisitiza ushirikiano na vyombo vingine vya dola hususani Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Askari Wahifadhi wamebainisha
changamoto mbalimbali wanazopitia katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni
pamoja na uchache wa Askari kulinganishwa na ukubwa maeneo yenye changamoto.
Pia, mashamba ya wananchi kulimwa
mbali mbali kati ya shamba moja na lingine kati ya umbali zaidi ya kilometa 5
imetajwa kuwa ni mojawapo ya changamoto zinazowawia ugumu Askari wahifadhi hao
kuwahudumia wananchi hasa pale
inapotokea mtawanyiko wa wanyamapori Katika maeneo yao na kushauri wananchi
walime mashamba yao kwa ukaribu ili iwarahisishie kuwapa huduma stahiki.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya
Tunduru Mhe. Simon Kemori Chacha amepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA na
Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa ujumla wilayani humo Katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na
waharibifu hususani tembo na kusisitiza
kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na
wanyamapori hao Kwa wananchi
Aidha, ametilia mkazo suala la ushirikiano baina ya Halmashauri, Taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na wadau wa uhifadhi Katika kutekeleza Mkakati wa Wizara wa kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.
Na. Beatus Maganja- Tunduru
0 Maoni