Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Orodha ya Wapiga Kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji huku akiwataka vijana wawe mstari wa mbele kushiriki zoezi hilo.
Amesema zimebaki siku nne tu, zoezi
hilo la uandikishaji lifikie ukomo Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo jana Kijijini
kwake Pwaga katika Tarafa ya
Kibakwe Mkoani Dodoma mara baada
kujiandikisha kwenye daftari hilo ambapo
amesema uchaguzi huo ni muhimu sana kwa
mustakabali wa maendeleo ya vitongoji na mitaa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mhe. Simbachawene
amewataka Wananchi kutofautisha
uandikishaji wa daftari la makazi
unaoratibiwa na TAMISEMI na ule wa
daftari la kudumu la wapiga kura unaoratibiwa
na Tume Huru ya Uchaguzj (INEC)
kwa ajili ya uchaguzi wa Mkuu wa mwaka ujao.
"Uchaguzi huu wa Serikali za
Mitaa una orodha yake ya wapiga kura na
uchaguzi ule wa kuchagua Diwani, Mbunge na Rais na wenyewe una daftari lake,"
amesisitiza Mhe Simbachawene.
Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene
amewahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la uandikishaji linaloendelea
nchi nzima huku akikisitiza kuwa yeyote ambaye hataweza kujiandikisha katika
daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hataweza
kushiriki kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi Novemba 27 mwaka huu.
Amesema uchaguzi huo ni muhimu sana
kwani unawapa fursa wananchi kuchagua vuongozi wanaoishi nao kwenye mitaa na
viongozi hao ndo msingi wa mchakato wa shughuli za maendeleo yanapoanzia.
"Msingi wa maendeleo ni watu, watu hao wakishirikishwa na wakiwa na viongozi wao na waliowachagua wataweza kupiga hatua za kimaendeleo kwani ndiko mawazo na ushirikishwaji wa mipango ya maendeleo yanapoanzia," amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Amewataka wananchi hao wajiandikishe
ili 27 Novemba mwaka huu waweze kuchagua viongozi badala ya kuwa watazamaji na
walalamikaji kwa kisingizio kuwa wao hawakuwachagua viongozi waliopo
madarakani.
Zoezi hilo la kujiandikisha lilianza
rasmi nchini kote kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka, huku rai kubwa ikitolewa kwa
wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao.
0 Maoni