Bunge wa Ludewa (CCM) Mhe. Joseph Kamonga ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kutenga asilimia thelathini ya fedha kwaajili ya kuviwezesha vikundi kazi vya kijamii ambavyo vinajishughulisha na matengenezo madogo madogo ya miundombinu wilayani hapo.
Pongezi hizo amezitoa mbele ya
waandishi wa habari mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya Ujumbe Maalum kutoka
Jamhuri ya Sierra Leone uliofika kujifunza namna vikundi vya kijamii
vinavyofanya kazi za ujenzi na matengenezo madogo madogo ya miundombinu ya barabara
katika Kata ya Lugarawa, Wilayani Ludewa.
Mhe. Kamonga alisema kwamba njia hiyo
ni namna bora inayofanywa na Serikali kupitia taasisi zake kwa kurudisha kipato kwa jamii na kwamba
imeleta ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuisaidia jamii kwani fedha hizo
zinawafikia watu wengi.
“Ninayo furaha kubwa sana ya kuwapokea
wageni hawa hapa Ludewa na wamejionea namna jamii inavyoshirikishwa katika
miradi ya Serikali kwenye ujenzi wa makaravati na matengenezo madogo madogo ya
barabara.”
“Tarura wamewapa mafunzo mbalimbali ya
namna ya kufanya matengenezo ya barabara, ujenzi wa makalavati pamoja na
madaraja, njia hii ni nzuri kwa serikali kurudisha mapato kwa jamii kwani
imeweza kuisaidia jamii kubwa kupitia kazi wanazofanya, tunawashukuru TARURA
kwa kuichagua Ludewa,” aliongeza Mhe. Kamonga.
Hata hivyo, Mhe. Kamonga alisema
kwamba TARURA katika jimbo lake wameweza kufungua barabara katika maeneo mengi
ambayo tangu Uhuru hakukuwa na barabara akitolea mfano barabara ya mwenge hadi
makonde hakukuwa na barabara kabisa ila hivi sasa wananchi wanayaona magari.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe.
Olivanus Thomas alisema kwamba TARURA imeweza kutumia zaidi ya bilioni 13
kwaajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini kwa kujenga barabara
za lami, changarawe na udongo katika
kipindi cha miaka mitatu chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wa ushirikishwaji wa jamii
alisema wilaya yake kuna vikundi vipatavyo hamsini na mbili ambavyo vinawajumlisha
wazee, vijana walemavu na wanawake ambavyo vimeweza kunufaika na fedha hizo
zilizotengwa kwaajili ya vikundi kazi.
“Yapo mazuri mengi ambayo yanafanywa
na Serikali nchi nzima kwani fedha za miradi zimepelekwa na kwa upande wetu
Ludewa kwenye upande wa TARURA zimeweza kuwanufaisha wakandarasi wadogo na
wakubwa kupitia pesa hizo.”
Aliongeza kusema kwamba kwa ujio huo
umekuwa na manufaa kwao kwani imekuwa ni historia kwa Tanzania hususan Ludewa
wageni wamejionea na kujifunza mambo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu
ya Sita kwa kufikia malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Olivanus
Thomas akiongea na Viongozi na wataalam mbalimbali kutoka Jamhuri ya Sierra
Leone na TARURA wakati walipotembelea vikundi vya kijamii wilayani Ludewa.
0 Maoni