Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amemtembelea na kuzungumza na Mzee
Yusuf Makamba leo, tarehe 25 Oktoba 2024, jijini Dar es Salaam.
Balozi Nchimbi alifika nyumbani kwa
Mzee Makamba, eneo la Wazo Hill, kumfariji kufuatia msiba wa mtoto wake, Bi.
Sakida Rajab Yusuf Makamba, aliyefariki dunia tarehe 12 Oktoba 2024, mjini
Morogoro.
Mzee Makamba, ambaye pia ni Katibu
Mkuu Mstaafu wa CCM, alimshukuru Balozi Nchimbi kwa kufika kumpatia pole na
alitumia fursa hiyo kumpongeza pamoja na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa (NEC) kwa juhudi zao katika kuimarisha chama.
“Sisi tunawaona, tunawasikia, na
tunawafuatilia. Endeleeni kuijenga na kuimarisha CCM. WanaCCM waendelee kufanya
kazi ya kujenga na kuimarisha chama kwa bidii zote. Hakuna mwingine
atakayefanya kazi hiyo bali wanaCCM wenyewe,” alisema Mzee Makamba.
Mapema kabla, Balozi Nchimbi, akiwa
ameambatana na Ndugu Issa Gavu, Katibu
wa NEC ya CCM Taifa - Oganaizesheni, alifika pia kuifariji familia ya marehemu
Balozi Jaka Mwambi, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu, kufuatia msiba wa mtoto
wake, Happiness Jaka Mwambi, aliyefariki dunia tarehe 24 Oktoba 2024, jijini
Dar es Salaam.
0 Maoni