Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amejiandikisha kwenye daftari la
wakazi katika mtaa wake, eneo la Kilimani, jijini Dodoma leo tarehe 18, Oktoba
2024.
Akizungumza baada ya kujiandikisha,
Balozi Nchimbi aliwasisitiza wananchi umuhimu wa kujitokeza kwa wingi
kuandikishwa, akisema kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha ushiriki wao
kwenye mchakato wa kidemokrasia.
Uandikishaji wa wapiga kura wa
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwenye daftari la wakaazi, ulianza tarehe 11
Oktoba, 2024 na utamalizika tarehe 20 Oktoba 2024.
Balozi Nchimbi amewahimiza wananchi
kutumia siku zilizobaki kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi bora
wa Serikali za Mitaa mwezi ujao, akisisitiza kuwa kila kura inahesabika na
inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii, ikizingatiwa kuwa viongozi
watakaochaguliwa watakuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya mitaa yao.
Balozi Nchimbi amesisitiza umuhimu
makundi yote katika jamii kushiriki kikamilifu, hususan vijana na wanawake,
kutambua nafasi yao ya kipekee katika mchakato huu, ikiwa pia ni sehemu muhimu
kwao kujihusisha na siasa kwa lengo la kuleta maendeleo katika jamii.
Pamoja na kuwasisitiza wananchi
wajiandikishe na kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, Balozi Nchimbi alisema
uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wenye
maono na uwezo wa kuongoza na kusimamia shughuli za maendeleo kama vile elimu,
afya, maji safi, na miundombinu.
Aidha, Katibu Mkuu ameendelea kuwataka
wananchi na wadau wote wa uchaguzi, kudumisha amani na mshikamano, kuepuka
kuchochea chuki katika jamii, na kuzingatia taratibu za kisheria, ili
kuhakikisha maslahi ya taifa na tija kwa wananchi, vinakuwa mbele, kabla,
wakati, na baada ya uchaguzi.
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Emmanuel John Nchimbi akiwa kwenye foleni wakati wa kujiandikisha daftari la wakazi katika mtaa wake, eneo la Kilimani, jijini Dodoma leo tarehe 18, Oktoba 2024.
0 Maoni