Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt.
Pindi Chana amekagua maboresho ya miradi mbalimbali ya kimkakati katika Hifadhi
ya Taifa ya Nyerere Mkoani Ruvuma.
Akiwa katika
ziara hiyo leo, Septemba 29, 2024 Mhe. Chana amekagua ujenzi wa kiwanja cha
ndege, lango la kitalii la kisasa, nyumba ya wageni yenye vyumba nane na ujenzi
wa nyumba za watumishi.
Akizungumza
katika ziara hiyo, Mhe. Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa katika sekta ya
Maliasili na Utalii ambapo alitoa fedha za UVIKO-19 zilizotumika kujenga miradi
hiyo.
Ametoa
maelekezo kwa TANAPA kuhakikisha lango la kitalii linaanza kutumika ili
kuiingizia Serikali mapato huku akipongeza ubora wa nyumba za Askari Uhifadhi
zilizojengwa katika eneo la Likuyu Sekamaganga.
"Tumepitia
nyumba watakazokaa askari wa Jeshi la Uhifadhi zipo kwenye hali nzuri kabisa na
nimeshatoa maelekezo geti lifanye kazi haraka kwa sababu limekamilika,"
Mhe. Chana amesisitiza.
Aidha, Mhe.
Chana ametumia fursa hiyo kuwaelekeza wawekezaji kukamilisha uwekezaji kwa
wakati.
"Kuna
watu wameshikilia maeneo katika maeneo yetu ya uhifadhi muda mrefu hakuna mtu
anaendeleza, hii inaikosesha Serikali mapato na ajira kwa vijana," amesema
Mhe. Chana.
Naye,
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya taifa Nyerere, Ephraim Anosisye
Mwangomo amesema kuwa miradi hiyo ya “Gate Complex” na Uwanja wa ndege
imegharimu takribani shilingi bilioni 2.1 kutokana na fedha za UVIKO-19.
Amesema
hifadhi hiyo imeendelea kupata wageni wengi kutoka nje na kuongeza mapato yake
hadi kufikia shilingi bilioni 11.9 kwa mwaka huu wa fedha ulioishia mwezi Juni
2024.
Hifadhi ya
Taifa ya Nyerere ni miongoni mwa hifadhi 21 zinazosimamiwa na Shirika Hifadhi
za Taifa Tanzania (TANAPA) na ina ukubwa wa kilomita za mraba 30,893 katika
mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Lindi na
Pwani.
0 Maoni