WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea
kusimamia ukusanyaji wa mapato nchini ambapo hali ya ukusanyaji wa mapato ya
ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kipindi cha mwezi Julai 2024
imeendelea kuimarika.
“Jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 113.701 kimekusanywa
sawa na asilimia 8 ya makisio ya mwaka 2024/2025 ya shilingi trilioni 1.356.
Aidha, makusanyo halisi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 90.665
yaliyokusanywa kipindi kama hicho cha Julai, 2023 ikiwa ni ongezeko la shilingi
bilioni 23.036.”
Ameyasema hayo leo (Septemba 6, 2024) wakati wa kuahirisha
Mkutano wa 16 wa Bunge, jijini Dodoma. “Ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya
ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, linachangiwa na mikakati mbalimbali
inayoendelea kufanywa na Serikali.”
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na usimamizi wa vyanzo
vya mapato vilivyopo, zoezi la mara kwa mara la ufanyaji tathmini ya vyanzo vya
mapato ya ndani ya kila Halmashauri kwa Halmashauri zote 184.
Waziri Mkuu amesema mkakati mwingine ni kutoa elimu ya
ulipaji ushuru kwa wananchi, pamoja na kuendelea kusimimamia matumizi sahihi ya
Mfumo wa TAUSI wa ukusanyaji mapato pamoja na mashine za kukusanyia Mapato -
POS.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema mwaka huu (2024) ni
mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajia kutafanyika siku ya
Jumatano, tarehe 27 Novemba, 2024, hivyo amewasisitiza kuwasisitiza Watanzania
wote kuwa tayari na kutimiza haki yao ya Kikatiba kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu
katika huo.
Amesema tayari uandaaji wa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa
mamlaka za serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa katika mamlaka
za wilaya na miji, mwongozo wa elimu ya mpiga kura na mwongozo wa uchaguzi wa
serikali za mitaa umekamilika.
“Nchi yetu imekuwa na utaratibu wa kujenga misingi ya
uongozi kuanzia ngazi za chini ili kuiwezesha Serikali kuwafikia watu wake
katika kutekeleza masuala mbalimbali ili kufikia azma kubwa katika kuleta
maendeleo endelevu.”
Amesema maandalizi mengine ya uchaguzi yapo katika hatua za
ukamilishaji ambayo yanajumuisha kutangaza orodha ya maeneo ya utawala, uhakiki
wa vituo vya kupigia kura awamu ya pili na manunuzi ya vifaa vya uchaguzi. “Kwa
sasa mamlaka husika zinaendelea na utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia vyombo
vya habari, mabango na mitandao ya kijamii.
“Kwa kuwa msingi wetu wa maendeleo unaanzia katika ngazi hii, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhakikisha tunatumia fursa ya mikutano yetu tuwapo majimboni, wasanii na vyombo vya Habari katika kutoa hamasa ya umuhimu wa wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.”
0 Maoni