Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Bahari na Uvuvi ya
Tume ya Umoja wa Ulaya, Bi. Charlina Vitcheva, anatarajiwa kutembelea Tanzania
kuanzia Septemba 9 hadi 11, 2024.
Ziara yake inalenga kushiriki katika Mkutano wa nane wa
Mawaziri Wanaohusika na Masuala ya Bahari, Maji ya Ndani, na Uvuvi kutoka
mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), ambao
utafanyika tarehe 11 Septemba katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere. Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya
Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ziara hii inaakisi dhamira ya Umoja wa Ulaya (EU) katika
kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika sekta ya uvuvi na uchumi wa
bluu. Hii ni ziara ya pili ya Vitcheva, ya kwanza ikiwa Novemba mwaka jana
amabapo, pamoja na shuguli nyengine, alikutana na kufanya mazungumzo Rais wa
Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Kabla ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa OACPS, Bi.
Vitcheva atatembelea Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) iliyoko
Kunduchi. Wakati wa ziara hiyo, ataangalia miundombinu ya utafiti ya taasisi
hiyo na kujifunza kuhusu jitihada za TAFIRI katika uhifadhi wa mfumo wa
ikolojia wa baharini. Aidha, atatembelea maonyesho yatakayobainisha shughuli za
uhifadhi za taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na maonyesho ya mbinu za kukusanya
data na utafiti mwingine wa baharini. Pia atahudhuria maonyesho ya kitengo
Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu, ili kujifunza kuhusu kazi yao ya
usimamizi wa bahari na juhudi za kusaidia ustawi wa jamii zinazoishi ndani ya
hifadhi za bahari.
Bi. Vitcheva pia atakutana na kampuni kadhaa changa za
Kitanzania zilizochaguliwa kupitia mpango wa Blue Invest Africa. Wawekezaji
hawa wanabuni suluhisho za kusaidia maendeleo endelevu kupitia ya uchumi wa
bluu.
Sehemu ya ratiba yake pia itajumuisha mkutano wa ana kwa ana
na Mh. Abdallah Ulega, Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania.
Ziara ya Bi. Vitcheva inaonyesha dhamira ya EU ya kuendeleza
uchumi wa bluu na usimamizi endelevu wa uvuvi nchini Tanzania. Msaada wa EU
nchini Tanzania unatekelezwa kupitia programu yake kuu ya TZS bilioni 332.5
(EUR milioni 110) ya Uchumi wa Bluu kwa Ajira na Mabadiliko ya Tabianchi.
Programu hii inalenga kujenga Uchumi wa Bluu unaohimili mabadiliko ya tabianchi katika miji ya pwani ya Tanzania, Zanzibar, na Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Hindi. Programu hii inadhamiria kujenga ulinzi wa mifumo ya ikolojia ya pwani, kukuza biashara endelevu zenye ajira nyingi, na kuhimiza ukuaji wa muda mrefu kupitia mageuzi ya sera na utawala wa mabadiliko.
0 Maoni