Watanzania 500 kusherekea siku ya Uhuru katika kilele cha Mlima Kilimanjaro

 

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na makampuni ya waongoza watalii nchini imepanga kuwapeleka watanzania zaidi ya 500 katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kusherehekea siku ya uhuru kupitia kampeni ya “Twenzetu Kileleni 2024” ikiwa ni msimu wa Nne wa Kampeni hiyo ikiwa na Kauli mbiu isemayo “Stawisha Uoto wa Asili Tanzania, Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro kampeni ambayo imezunduliwa leo mpaka disemba 4, 2024.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Jully Lyimo amewaeleza wanahabari katika mkutano na vyombo vya Habari uliofanyika katika ofisi za TANAPA jijini, Dar es Salaam leo kuwa lengo la kampeni hii ni kusherehekea miaka 63 ya Uhuru, tukio ambalo ni la kihistoria hufanyika kila mwaka ifikapo Desemba 9.

“Katika sura ya Utalii, TANAPA imekuwa ikitumia fursa hii ya maadhimisho ya siku ya uhuru kuhamasisha watanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kutangaza vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hii kupitia kampeni ya “Twenzetu kileleni” .Lengo la kampeni hii ni kuhamasisha Watanzania kupanda mlima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika.”

“Nichukue nafasi hii kuwahamasisha Watanzania wenzangu kushiriki upandaji huu ikiwa ni kuonyesha uzalendo na kupenda vivutio vyetu. Kwa hivyo kwa mwaka huu ni msimu wa nne wa kampeni hiyo, tunatoa hamasa kwa watu binafsi, watanzania ndani na nje ya nchi, mabalozi, taasisi za Serikali na binafsi kujitoa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizi.”

"Kama tulivyofanya mwaka jana jumla ya kampuni tatu ndio zimejitokeza kushiriki kampeni hii katika msimu huu wa nne Kampuni hizo ni ZARA Tours, African Zoom na African Scenic," alisema Kamishna Lyimo.

Kampuni ya ZARA TOURS itatumia njia ya Marangu kama ilivyozoeleka, African Zoom watatumia njia ya Machame na African Scenic watatumia njia ya Lemosho ambapo idadi ya siku za kupanda mlima huo ni 6 kwa njia ya Marangu.

Aidha, siku 7 kwa njia ya Machame na kwa Lemosho itakuwa siku 8 huku Gharama za kupanda mlima zitakuwa ni shillingi 1,55,000/- kwa njia ya Marangu, shillingi 1,830,000/- kwa njia ya Machame na 2,000,000/- kwa njia ya Lemosho, aliongeza Kamishna Lyimo.

Afisa Uhifadhi Mkuu Mapinduzi Mdesa kutoka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliwataka watanzania wote kujitokeza katika kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika pamoja na kushiriki katika juhudi za kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro.

"Kama mwenyeji wa mlima niwakaribishe watanzania kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika lakini tunajukumu la kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro kwa kustawisha uoto wa asili kwenye maeneo yetu.”

Aidha, Mdesa aliongeza kuwa tafiti zinaonyesaha kuwa chanzo cha barafu kuyeyuka Mlima Kilimanjaro ni uwepo wa pepo kavu zinazotokea baharini na maeneo mengine ya nchi zikifika kwenye ile barafu ya Mlima Kilimanjaro zinapelekea Barafu ile kupungua ukubwa wake na kutoa rai ya kukijanisha Tanzania kwa kupanda miti ya asili ili pepo zinazotoka kwenye fukwe ziende na unyevu na kusaidia barafu iendelee kuwepo.

Historia inaonyesha kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961. Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kille cha Mlima Kilimanjaro.

Tukio hili limekuwa likihusisha kikundi cha wanajeshi wachache wakishirikiana na askari wa Hifadhi za Taifa Tanzania kwa utaratibu wa kampuni ya utalii ya ZARA ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita maadhimisho haya yalipata sura mpya ya ushiriki wa wananchi na kutambulika kwa jina la "Twenzetu Kileleni" ambapo kwa sasa ni msimu wa nne.

Na.Edmund Salaho- Dar es Salaam


Chapisha Maoni

0 Maoni