Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kulinda
na kudumisha amani iliyopo nchini kwa kuzingatia misingi ya upendo, uvumilivu
na kuheshimiana.
Dkt. Biteko
ameyasema hayo leo Septemba 21, 2024 jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory
Mpango katika Kongamano la Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT)
katika Siku ya Amani Duniani inayolenga kuifanya dunia kuwa sehemu sala ya
kuishi kwa kuhimiza kutunza thamani ya amani na kuzuia migogoro.
Aidha,
amewaasa Watanzania kudumisha amani iliyopo nchini ili kutoa fursa kwa nchi na
Watanzania kujiendelea kujiletea maendeleo.
Dkt. Biteko
amesema kuwa licha ya Mwenyezi Mungu kuibariki nchi ya Tanzania kwa kuwa na
eneo kubwa lenye rasilimali pamoja na watu wenye tofauti za imani, kipato na
makabila bado ni lazima Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kutunza amani kwa
kuwa ni msingi wa maisha.
‘’Mungu
ametuumba akatuweka katika nchi nzuri na kubwa yenye mita za mraba zaidi ya
900,000, akatupa milima, mabonde na tambarare, Mungu ametupa matabaka ya wenye
navyo na wasio navyo, tofauti za umri, makabila, akatuunganisha nchi mbili
Zanzibar na Tanzania Bara kuwa nchi moja haya yote yamewezekana na tofauti hizi
hazijatupa haja ya kuondoa amani yetu. Tofauti tulizo nazo ni nyingi lakini
zisiwe sababu za kutofautiana na kuondoa amani yetu,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza
kuwa ikiwa dini moja au kabila moja likajiona bora kuliko linguine hali hiyo
itasababisha uvunjifu wa amani, na kuwa Watanzania wanahitaji kustahimiliana
ili kujenga amani ya pamoja.
‘’Amani
ikitoweka wanaoumia si tu wanaosababisha itoweke bali hata wewe unayedhani
haikuhusu mataifa yenye migogoro wanatumia fedha za wananchi kwenda kutafuta
amani kwa kujadiliana katika nchi zingine, hivyo tuilinde nchi yetu,’’ amebainisha
Dkt. Biteko.
Fauka ya
hayo, Dkt Biteko ameitaka JMAT kuwa sehemu ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa
wananchi kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27,
2024 kwa kuhimiza wananchi kugombea na kuchagua viongozi wenye sifa. Aidha,
amesema kuwa uchaguzi huo uwaunganishe Watanzania kwa kufanya kampeni za
kistaarabu na wagombea kuelezea tofauti zao za mawazo kistaarabu.
Naye, Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,
Amoni Mpanjo amesema kuwa amani ni nguzo kuu ya kila jambo na ndio maana Wizara
inahimiza amani ndani ya jamii. Aidha, ameipongeza JMAT kwa kuunganisha dini na
watanzania na kusema Jumuiya hiyo ni mbia kwa Wizara yake na inasaidia
kuwafikia Watanzania, Sambamba na kuasa jamii kuacha vitendo vya ukatili
ikiwemo utekaji na ubakaji.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum
amesema kuwa lengo la Kongamano hilo la JMAT ni kuiombea nchi ili wanaofanya
vitendo vya kihalifu kuacha na wananchi
waishi kwa amani na bila hofu.
‘’Sisi
viongozi wa dini tunaamini kupitia maombi amani itaendelea na vitendo viovu
vitaisha mafundisho ya dini zetu yote yanatufundisha kuhusu amani,’’ amesema
Sheikh Alhad.
Mkurugenzi
Idara Kuu ya Fedha, Uchumi na Utekelezaji wa
JMAT, Bw. Ayub Sanga amesema kuwa Jumuiya hiyo inashughulika kwa ajili
ya amani na maridhiano na inahusisha dini zote ikiwemo Budha na Hindu na kuwa
viongozi wake wanatoka katika dini mbalimbali pamoja na viongozi wa mila na
desturi ili kupangana vizuri kwa ajili ya kuendelea kudumisha amani nchini.
0 Maoni