Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula ameitaka Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kusimamia kikamilifu shughuli za utalii ili
kulinda kazi iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza sekta hiyo kimataifa na kuongeza idadi
ya watalii nchini.
Mheshimiwa
Kitandula ametoa kauli hiyo mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili
mwishoni mwa wiki aliyoifanya ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kukagua miundo
mbinu ya barabara na kuzungumza na menejimenti ya Mamlaka hiyo ikiongozwa na
Kamishna wa Uhifadhi Dkt. Elirehema Doriye.
Amesema
kwamba katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuwa
kivutio bora duniani ni vema ikaongeza nguvu katika kuboresha miundo mbinu ya
barabara ambapo itasaidia kuimarisha shughuli za utalii na kuongeza idadi ya
watalii.
“Kazi kubwa
ya kutangaza utalii imefanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo
ni jukumu letu kusimamia kazi hiyo na tusikubali kurudi nyuma,imarisheni miundo
mbinu ya utalii ili nchi yetu iendelee kuwa na sifa kubwa kimataifa,”alisema
Naibu Waziri Kitandula.
Kwa upande
wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema
Doriye alimhakikishia Naibu Waziri Kitandula kwamba Mamlaka itayafanyia kazi
maelekezo yote ili kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua na hivyo
kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Katika ziara
yake hiyo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dunstan Kitandula
alitembelea barabara ya Loduare mpaka
Golini kuelekea Serengeti, Barabara ya Ndutu kuelekea Endulen,Barabara ya
Olduvai kupitia Golini na alipata nafasi pia ya kukagua ujenzi wa jengo la
makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lililopo pembezoni mwa mji wa
Karatu.
0 Maoni