Ujenzi wa
Barabara ya Iringa - Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami uliogharimu takribani
shilingi bilioni 142.56 utasaidia kukuza
utalii wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kurahisisha ufikaji wa watalii katika
hifadhi hiyo.
Hayo
yamesemwa leo Septemba 21, 2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi,
Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati wa hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya Ujenzi na
Usimamizi wa Barabara ya Iringa-Msembe
kiwango cha lami iliyofanyika leo Septemba 21,2024 katika Uwanja wa
Samora, Mkoani Iringa.
“Ujenzi wa
barabara ya hii pamoja na mambo mengine utasaidia kuongeza idadi ya watalii na hasa Utalii wa ndani na
kukuza pato la Taifa, haya ni mafanikio makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza Mhe. Chana.
Ameongeza
kuwa mradi huo pia utasaidia kufungua
fursa za upatikanaji wa huduma za kijamii
na kukuza uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa huku akiwataka
wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Hifadhi mbalimbali za Nyanda
za Juu Kusini.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amesema
Barabara hiyo pamoja na mambo mengine itatoa mchango mkubwa katika shughuli za
utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyopo Mkoani Iringa.
"Utalii
ili uweze kustawi lazima miundombinu iwepo hivyo barabara hii itakuza utalii
ikiwa ni fedha ambazo Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kujengwa kwa Barabara hii," amesema.
Hafla hiyo
imehudhuriwa na Wabunge wa Mkoa wa Iringa, Viongozi mbalimbali wa Chama na
Serikali, Watendaji na Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na
wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Na. Happiness Shayo - Iringa
0 Maoni