Serikali
imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii
inayojitegemea chini ya Wizara yenye dhamana ya masuala ya Ustawi wa Jamii ili
kurahisisha na kuimarisha uratibu, usimamizi na utekelezaji wa afua za Ustawi
wa Jamii nchini.
Hayo
yamesemwa jana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifunga Mkutano wa tatu wa Mwaka wa
Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri Dkt.
Gwajima amesema lengo la kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii itakayojitegemea ni
ongezeko la uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii kisekta kunakohitaji Taasisi
madhubuti katika kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hizo katika jamii
kupitia Taasisi za umma, binafsi na wananchi kwa ujumla.
Amebainisha
kwamba, hatua hiyo ni matokeo ya kukubaliwa kwa wasilisho la mapendekezo ya
Haki Jinai kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ambapo mpango huo kwa sasa unasubiri maelekezo ya muundo wa Idara hiyo
kupitia Wizara ya Utumishi.
"Namshukuru
sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii namba moja kwa kutambua mchango wa kazi
zenu na kuipa kipaumbele tasnia hata kubariki tuendelee kufanya mkutano huu
kila mwaka ili kupata nafasi ya kujifunza mambo mazuri kutoka kwa wenzetu na
kujadili namna ya kutatua changamoto za ukatili wa aina mbalimbali zinazoikumba
jamii yetu kwa sasa pamoja na namna ya kuboresha mazingira ya kazi tunapotekeleza
majukumu yetu," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt.
Gwajima amesema elimu itakayotolewa na Maafisa hao itasaidia jamii kuelewa
mambo mbalimbali ya huduma za kiustawi hasa huduma za unasihi kwa watoto,
wazazi/walezi, huduma za uchangamshi wa awali ya watoto wadogo na huduma ya
Afya ya Akili na Msaada wa Kisaikolojia na kijamii kwa makundi yenye uhitaji.
Aidha,
amesema Familia ndio taasisi pekee ambayo ni nguzo muhimu katika malezi bora
inayomuandaa mtoto kuwa mwanaume au mwanamke bora wa baadaye na familia ndiyo
mahali salama kwa watoto kukua na kufikia utimilifu wao hatimaye kuwa raia
wema, wenye maadili na wazalendo watakaochangia ustawi waTaifa letu hivyo ni
lazima kuwekeza katika kutoa elimu ya umuhimu wa familia kwa wazazi na walezi.
Waziri Dkt.
Gwajima ameongeza kwamba, familia zimekuwa zikikukumbwa na changamoto nyingi
ikiwemo umaskini, migogoro ya ndoa na familia, malezi duni kwa watoto
inayopelekea kukosekana kwa muunganiko na mahusiano hafifu kati ya wazazi au
walezi na watoto wao, ambapo athari zake ni pamoja na watoto kukosa upendo wa
wazazi au walezi.
Ameeleza
kuwa kuendelea kuwepo kwa mila na
desturi za kukaa kimya na kuficha taarifa za vitendo vya ukatili hasa
vinavyotokea ndani ya familia imesababisha kuendelea kuwepo kwa vitendo vya
ukatili na kukosekana huduma kwa wahanga hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili na tabia hatarishi kwa
watoto.
Kwa upande
wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amewapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii kwa msisitizo
wana mchango mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Naye
Mwenyetiki wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe.
Fatma Tofic amesema, anatambua kuwa Wataalam hao wamefanya tathimini ya mambo
yote yanayotakiwa ili kuboresha utendaji kazi zao na kutatua changamoto zao,
ambapo Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kuongeza Bajeti ili
kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Mkutano wa
tatu wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wenye kaulimbiu “Tanzania Bila Ukatili
Inawezekana, Imarisha Mahusiano Ndani ya Familia” umefanyika kwa muda wa siku
tatu, Septemba 18 – 20, 2024 Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
0 Maoni