Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko ametoa rai kwa vijana nchini kuwa na mshikamano na kudumisha iliyopo
amani nchini.
Dkt. Biteko rai hiyo leo Septemba 20, 2024 jijini Dar es
salaam wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Ajenda ya Amani
na Usalama kwa Vijana.
‘’Wito wangu kwenu shikamaneni shikamaneni shikamaneni! kwa
ajili ya kulinda amani ya nchi yetu ili tuwe na Taifa la utulivu na tufurahie
maisha yetu, ni vizuri mkakumbuka kuwa hiki ni kipindi cha kujiandaa kuwa baba
bora au mke mwema ili baadae kuwa na Taifa bora,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.
Akizungumzia maendeleo ya utandawazi na mapinduzi makubwa ya
kidijitali ambayo yamekuwa yakitoa fursa lukuki kwa Vijana, Dkt. Biteko amesema
‘’Napenda kuwaasa kwamba matumizi ya teknolojia yakawe na malengo ya kuzalisha
na kujitengenezea kipato endelevu, kwa kufanya hivyo kutakuza uchumi na
kuonyesha tija ya nguvu kazi yetu katika Taifa letu. Aidha, siyo teknolojia hii
inavyotumika sasa kama majukwaa ya uhalifu, uchochezi, udhalilishaji wa
kijinsia na uvunjaji wa amani iliyojengwa na vizazi vya Watanzania wengi.
Natamani Baada ya Kongamano hili nyie wote mlioudhuria hapa mkawe chachu kwa
vijana wenzenu mtakao kutana nao, mkawe dira na walimu bora wa amani,’’amesema
Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko ameongeza
kuwa katika kuhakikisha
kunakuwepo na mazingira mazuri ya ushiriki na ushikikishwaji wa vijana
katika masuala mbalimbali ya maendeleo
Serikali imefanyia maboresho Sera ya zamani Maendeleo ya Vijana na
tarehe 12 Agosti 2014 Sera Mpya ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007, tolea la
mwaka 2024 ilizinduliwa.
‘’Sera hii imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha
vijana wanaandaliwa kuwa wazalendo, waadilifu na wanaoshiriki kudumisha amani
na usalama wa nchi yetu. Hii yote ni kutambua umuhimu na nguvu waliyonayo
vijana na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika katika kujenga nchi yetu. Katika
kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 ninawasihi kuwa tumieni fursa hii kuhakikisha mnatoa maoni yenu
ambayo pamoja na mambo mengine yatawezesha ushirikishwaji wa vijana kwenye
kwenye maendeleo, lakini hasa katika misingi ya amani na usalama na mtumie
ubunifu wenu kupendekeza mikakati rafiki kwa vijana itakayowawezesha kushiriki
kujenga aina ya Tanzania tuitakayo miaka 25 ijayo, ’’ amesisitiza Dkt. Biteko.
Inaelezwa kuwa takribani asilimia 34.4 ya idadi ya
Watanzania wote ni vijana ambao ni sawa na asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa
na asilimia 46 ya idadi ya watu wote duniani ni vijana walio chini ya umri wa
miaka 25.
‘’Wote mtakuwa mashahidi kinachoendelea duniani kote, amani
imepungua, vifo vimeongezeka, matukio ya uovu yamekithiri na baadhi ya mataifa
hayana amani kwa sababu yana migogoro na mivutano ya kisiasa. Ni vyema
mkatambua kwamba ninyi vijana wa Tanzania pamoja na wenzenu duniani kote mna
jukumu kubwa la kutoa hamasa ya kushiriki katika kujenga na kuilinda amani, na
msimruhusu mtu yoyote kuichezea tunu hiyo muhimu kwenye mustakabali wa Taifa
lolote Duniani,’’ amemalizia Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa
Umoja wa Mataifa Tanzania, Shabnam Malick amesema kuwa Shirika hilo litaendelea
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufadhili programu mbalimbali
kuhusu vijana kwa kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo
nchini.
‘’Tunaamini kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na
msingi wa maendeleo endelevu ni lazima tushirikishe vijana katika kufanya
maamuzi,’’ amesema Bw. Malick.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la A.L.I.I na Mratibu wa
Kongamano hilo la Vijana, Bw. Joseph Malekelea amesema kuwa Kongamano hilo
limefanyika kuendana na maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani linalofanyika
Septemba 21 kila mwaka lilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kukumbusha watu,
mataifa na wadau mbalimbali umuhimu wa kudumisha maadili ya amani na usalama.
‘’Tanzania tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo na kwa ubunifu
wetu tukamua kuandaa Kongamano hili ili tuweze kuona kwa kina je vijana wetu
wanaelewa kuhusiana na amani, je wanashiriki katika kudumisha amani katika nchi
yetu, je vijana wetu wanashirikishwa katika suala zima la amani, kipi kifanyike
kuhakikisha vijana wanakuwa mstari wa mbele katika kudumisha aman,’’ amesema
Bw. Malekela.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu “KIJANA CHUKUA HATUA KUDUMISHA UTAMADUNI WA AMANI TANZANIA.” Limefanyika sambamba na utoaji wa elimu katika shule mbalimbali kuhusu kudumisha utamaduni wa amani kupitia midahalo ya vijana na mbio za amani katika mikoa ya Tanga, Mjini Magaribi – Zanzibar, Pwani, Lindi na Mtwara na kuwafikia zaidi ya vijana 10,000.
0 Maoni