WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea
kujiimarisha kidiplomasia na itaongeza nguvu zaidi ili kuwawezesha Watanzania
wengi kupata fursa mbalimbali katika jumuia za kimataifa.
Amesema Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
imefanikisha kuimarisha ushirikiano baina ya nchi washirika na sasa mafanikio
yanaonekana.
"Rais wetu
ameonesha nia njema katika kipindi chake cha miaka mitatu na nusu amefanya kazi
kubwa ya kujenga diplomasia na mahusiano katika sekta mbalimbali na nchi nyingi
duniani."
Ameyasema hayo leo
(Jumatano, Agosti 4, 2024) alipokutana na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la
Afya Duniani kanda ya Afrika (WHO) Dkt Faustine Ndungulie, Ofisini kwake Mlimwa
Jijini Dodoma.
Jitihada hizo za
Serikali ya awamu ya sita zimeiwezesha Tanzania kuendelea kupaa kidiplomasia
kuiwezesha nchi kupata viongozi wakubwa ndani ya Taasisi za kimataifa.
"Tunaamini kazi
kubwa tulizozifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kumpata spika wa
Umoja wa Mabunge duniani haikuwa kazi ndogo, na tena tumepata Mkurugenzi wa
Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika."
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea
kumuunga mkono Mkurugenzi huyo katika
utekelezaji wa majukumu yake mapya.
"Wakati wote
Waziri wa Afya atakuwa karibu nawe kuhakikisha kwamba sera zetu zinaenda
sambamba na malengo ya WHO, kwa uwepo wako sisi lazima tuwe msitari wa mbele
kuhakikisha kwamba tunakuunga mkono kwa mipango yetu ya afya ndani ya
nchi."
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo Mtarajiwa wa Shirika la Afya
Duniani Kanda ya Afrika DKT. Faustine Ndungulile amemshukiru Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kumuunga mkono na kufanya ushawishi wa kidiplomasia ili
kufanikisha ushindi huo.
"Kwa upekee sana ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa katika kufanikisha ushindi huu kwa ushawishi wake kwenye jumuia za kimataifa pia nawashukuru viongozi wengine wa Serikali, Bunge na wadau wote."
0 Maoni