Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na viongozi wa dini ili
kuwawezesha kutimiza majukumu yao ya kitume kwa maendeleo ya Watanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 17, 2024 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Dayosisi ya Mwanga, Kanisa Kuu lililopo Mkoani Kilimanjaro wakati akitoa salamu
za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan mara baada ya ibada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu wa
Dayosisi hiyo, Chediel Sendoro.
Askofu Sendoro amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea
Septemba 9, 2024 katika eneo la
Kisangiro wilayani Mwanga.
“Rais yupo tayari kushirikiana na kanisa wakati wowote ili
kanisa liweze kufanya kazi zote za kitume na sisi tuko tayari kuifanya Tanzania
iwe bora na Watanzania waishi vizuri katika nchi yao,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa msingi wa Dayosisi hiyo umejengwa kwa upendo
na kuwa moja ya kazi kwa viongozi wa kanisa hilo ni kupata mtu atakayeendeleza kazi na maono ya Askofu
Sendoro juu ya kanisa hilo.
Amefafanua kuwa kila binaadamu ataiaga dunia itakapofika
wakati wake ispokuwa kila mmoja aliyehai amefanya nini na hivyo hawana budi
kukumbuka mahubiri ya Askofu Sendoro na umoja alioujenga miongoni mwao.
“Natoa pole kwa familia, wazazi, mjane, watoto na wajukuu
kwa kuwa Septemba 9, 2024 lilitokea jambo lisilo la kawaida na kuondokewa na
Askofu Sendoro. Nakupa pole Askofu Mkuu wa Kanisa, maaskofu wote na Wanamwanga,
tuyaenzi yote aliyokuwa akiyaishi,
alijali sana maadili yetu naomba tena tuendelee kuliombea Taifa na nchi yetu,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Rais Samia alishatoa
muongozo na uchunguzi ufanyike haraka iwezekanavyo juu hali ya siasa na vitendo
vya uvunjifu wa amani nchini. “Nataka niwaombe kama viongozi wa kiroho muendelee
kushirikiana na Serikali kuwaombea Watanzania na kuifanya Tanzania kuwa mahali
bora zaidi pakuishi.”
Akihubiri katika ibada hiyo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri, Askofu Dkt. Alex Malasusa amesema kuwa siku ya leo ni siku ya pekee
ambayo Askofu Sendoro amelala kwenye jeneza na kuwa ni jambo ambalo kibinadamu
linatisha lakini hakuna kitakachoweza kuwatenga na tendo la Mungu.
“Hata katika hili Mungu anaonesha pendo lake, wazazi wake na
watoto wake endeleeni kuamini Mungu ameonesha pendo lake, watu wa Mwanga mlikua
na Askofu endeleeni kuliangalia pendo la Mungu msiliangalie hili gumu
lililotokea angalieni pendo lake,” amesema Askofu Malasusa.
Amesititiza “Nachotaka kukazia hapa kile tunachosema hasa
sisi wachungaji kionekane katika maisha yetu, matendo yetu na kuishi kwetu.
Mtakatifu Paulo anatufundisha kuwa yuko pamoja nasi, tuangalie alama ya msalaba
ni alama ya ushindi.”
Aidha, Askofu Malasusa amewaeleza waombolezaji kuwa walio hai wanapaswa kuishi maisha ya
uhakika ili Mungu atakapowaita wawe tayari na kuwa na ushuhuda wa kweli sio wa kusemwa na watu, na
kuwa waendelee kuliombea kanisa.
Askofu Malasusa ametumia jukwaa hilo kuwataka Watanzania
kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye waka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika mwakani.
Aidha, amewataka viongozi wa kisiasa kukutana na kuzungumza
juu ya changamoto zinazowakabili ili nchi iendelee kuwa na amani na mahali
pazuri pa kuishi.
Akitoa salamu, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu
Mstaafu, Mzee Cleopa Msuya amewataka wana Mwanga na KKKT kwa ujumla kumuenzi
Askofu Sendoro kwa kuendeleza misingi imara aliyoijenga.
Amesema licha ya machungu waliyonayo waumini wanapaswa
kujipanga na kupata viongozi watakaotimiza malengo yake juu ya kanisa hilo.
“Niombe watakaotafuta mbadala wake watupatie mtu ambaye yale
yote aliyoanzisha yataendelea na kutuunganisha wakristo hapa Mwanga na Dayosisi
zingine. Tafuteni mtu atakaye vaa viatu vya Askofu Sendoro,” amesema Mzee
Msuya.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph
Tafayo amesema “Nazungumza kwa niaba ya wananchi wa wote wa Mwanga kwa sababu
yalipotokea matatizo mbalimbali Askofu Sendoro alishirikiana nasi watu wa
Mwanga.”
Ameendelea kwa kusema kuwa Baba Askofu huyo aliwashirikisha waumini wa kanisa hilo katika shughuli mbalimbali wakati wa uongozi wake na kwa muenzi kwa wataendelea kushirikiana na uongozi wa Kanisa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanga Dkt. Chediel Elinaza Sendoro katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mwanga, Kanisa Kuu lililopo Mkoani Kilimanjaro.
Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Cleopa Msuya akiongea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mwanga, Kanisa Kuu lililopo Mkoani Kilimanjaro wakati wa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Chediel Elinaza Sendoro.
0 Maoni