Askofu Malasusa akemea vitendo vya mauaji na utekaji nchini

 

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amesema kanisa linasikitishwa na hali inayoendelea hivi sasa ya utekaji na kutoweka kwa watu, inayotishia amani na utulivu nchini.

Askofu Dkt. Malasusa ametoa kauli hiyo leo Septemba 17, 2024, katika Ibada ya Maziko ya Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, marehemu Dkt. Chediel Elinaza Sendoro, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mwanga Mjini.               

Dkt. Malasusa amesema, mauaji ni laana kama inavyoonywa katika Biblia, na hivyo ni vyema hali hiyo ikakomeshwa ili nchi isiingie katika laana. Ameishauri Serikali kuruhusu meza ya majadiliano kuzungumzia utekaji huo ili kupata suluhisho la kudumu la kukomesha mashaka hayo yaliyopo sasa katika jamii.

Aidha, Askofu Dkt. Malasusa ameagiza Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa hilo, kuwa na maombi maalum katika Ibada kama jambo maalum katika nyakati hizi ili kumlilia Mungu aliepushe Taifa na laana hiyo.

Askofu Dkt. Chediel Elinaza Sendoro alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Septemba 9, 2024 katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Chapisha Maoni

0 Maoni