Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba amewataka Wataalam wa
Ustawi wa Jamii mchini kwa kushirikiana na wadau kuandaa na kutekeleza mkakati
wa kuwaondoa Watoto wanaoishi na kufanya Kazi Mitaani ngazi ya Taifa.
Maelekezo hayo yametolewa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa
Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa
Ustawi wa Jamii jana Septemba 18, 2024 mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro.
Mhe. Chande amesema mkakati huo uendane na mpango wa
ufuatiliaji na mikakati itakayoandaliwa ngazi ya Mikoa na Halmashauri, huku
Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau kuendelea kutoa elimu ya
malezi chanya kwa jamii ili kuwa na nguvu kazi yenye tija kwa Taifa.
Amewaasa pia Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao
kwa uadilifu kwa kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
"Mikoa na Halmashauri muandae na kutekeleza Mpango
mtambuka wa kuzuia na kushughulikia ukatili dhidi ya watoto, ukatili wa
kijinsia na tatizo la Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mitaani utakaojumuisha
kutengeneza nyaraka ya mkakati wa Mikoa ambayo taarifa yake itawasilishwa
kwenye vikao vya Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mikutano ya
Wataalam wa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Biashara, Sheria, Kilimo,
Utalii, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi, Makamanda wa Mikoa," amesema Mhe.
Chande.
Aidha, mewaahidi wataakam hao kulifanyia kazi suala la
kuweka afua ya Ustawi wa Jamii na kuainisha kwenye Mwongozo wa Bajeti kwa Mwaka
2025/26 kama zilivyoainishwa afua zingine na kuweka mgao wa 3% ya bajeti ya
kutekeleza.
Ameziomba pia Ofisi za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha
zinatenga Ofisi za Ustawi wa Jamii zenye vyumba vya kutosha kutoa huduma kwa
kuzingatia faragha, kuanzisha huduma ya nyumba salama kwa ajili ya kuhifadhi
wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na kuendelea
kuimarisha utambuzi na usajili wa Watu Wenye Ulemavu ili kuwezesha utoaji wa
huduma stahiki.
Kuhusu Elimu kwa Umma, amesema kila Halmashauri iandae na
kutekeleza mpango na huduma mkoba kwenye jamii na Mkoa kutoa taarifa ya kila
robo mwaka kwenye Mamlaka husika na wakati wa mkutano wa mwaka wa Maafisa
Ustawi wa Jamii.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamìi, Jinsia na
Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amesema Serikali itaendelea kusuluhisha
migogoro ya ndoa kupitia Baraza la usuluhishi, jumuiya, kata pamoja na Maafisa
Ustawi wa jamii katika mamlaka za serikali za mitaa.
Mhe. Mwanaidi ametoa takwimu za migogoro 74349 ya ndoa iliyotatuliwa ambapo mashauri
ya ndoa na matunzo ya watoto 49, 302
sawa na asilimia 14.7 , yaliyatuliwa,
matunzo ya watoto nje ya ndoa 25017 sawa na asilimia 18.1 yaliyoripotiwa na
yaliyo mahakamani ni 4,551.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na
Maendeleo ya jamii Fatma Toufiq amewapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii kwa
kufanya kazi karibu na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali bila kujali
changamoto mbalimbali wanazozipitia katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa
elimu kuhusu ukatili katika jamii.
Amesema hali ya ukatili inazidi kwenye jamii hivyo kuna kila sababu ya kujiuliza tumekosea wapi mpaka vitendo vya ukatili vinazidi? . Ameongeza kuwa wataendelea kuishauri Serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwalinda watoto.
0 Maoni