Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
imeendelea kutimiza ahadi ya kugawa chakula kwa wananchi waliotoka eneo la
hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia kijiji cha msomera kwa kuwapa gunia 2 za
mahindi kila kaya ambapo mpango huo hufanyika kila baada ya miezi mitatu kwa
kipindi cha miezi 18 wakiwa wanaendelea kuzoea mazingira.
Akiongoza zoezi la ugawaji wa mahindi jana tarehe 18/09/2024,
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi anayesimamia idara ya Maendeleo ya
Jamii Gloria Bideberi, alisema kuwa zoezi la ugawaji wa mahindi kwa wananchi
hao ni endelevu na linafanyika kila baada ya miezi mitatu kwa kadri wananchi
wanavyoendelea kuhamia katika Kijiji cha Msomera.
“Sisi kama Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tunaendelea na
utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mwananchi wa
Ngorongoro aliyehamia Msomera pamoja na nyumba na huduma nyingine ambazo
anapewa na Serikali, tunahakikisha pia anapatiwa Mahindi jumla ya magunia 12
kwa muda wa Miezi 18 ya mwanzo akiwa
bado anajipanga kuandaa shamba alilopewa” alisema Kamishina Gloria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Wakili Abert
Msando ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa mahindi kwa wananchi hao ni mpango wa
Serikali wa kuhakikisha kuwa wanachi wote wanaohamia Msomera wanapatiwa maisha
bora zaidi tofauti na walikotoka ambapo sheria za uhifadhi zinawabana kufanya
baadhi ya shughuli kama kilimo.
“Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanapofika
Msomera wanapatiwa mahindi ili kuwawezesha kujipatia chakula wakati wakiwa wanajiandaa
na msimu wa kilimo kwenye eneo la ekari 2.5 lililopo kwenye nyumba
aliyokabidhiwa na Serikalai na ekari zingine tano ambazo amepewa mahsusi kwa
ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali,” alisema Mhe. Msando.
Bw. Sabore Olemoko ambaye ni mmoja kati ya wananchi
wanaonufaika na program hiyo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na
kubainisha kuwa wanafurahia maisha wanayoishi Msomera hasa kukuta huduma zote
muhimu za kijamii na fursa za kiuchumi ambazo serikali imewaahidi.
“Tunapenda kuishukuru Serikali yetu kwani baada ya kuhamia
Msomera tumenufaika kwa vitu vingi kama vile mashamba, nyumba, zahanati, maji,
shule, mabwawa, maeneo ya malisho, minada na leo tupo hapa tunapokea mahindi
kwa ajili ya chakula cha familia zetu amnacho kinatusaidia kwa wakati huu ambao
tunasubiri msimu wa kilimo uanze ili tuanze kulima mazao mbalimbali na kuanza
kujitegemea kama wenzetu ambao walitangulia miaka miwili iliyopita,” alisema
Bw. Sabore.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambapo hadi kufikia tarehe 18 septemba, 2024 jumla ya kaya 1451 zimenufaika na mgao wa mahindi takribani tani 945 kwa awamu tofauti.
0 Maoni