Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameshuhudia
Utiaji Saini wa Mikataba ya usambazaji na utoaji wa huduma mgodini katika mgodi
wa uchimbaji Madini ya Urani uliopo katika Kijiji cha Likuyu kilichopo Wilaya
ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Mikataba hiyo imesainiwa jana ambayo imehusisha Kampuni ya
Ako Group Tanzania Limited ambayo ni mzabuni wa Kampuni ya Mantra na vikundi
vilivyoundwa na wazawa vitakavyo toa mahitaji mbalimbali kwa mzabuni huyo. Ako
Group wanatoa huduma ya chakula na usafi katika mradi huo, hivyo mikataba hiyo
itasaidia ununuzi wa mahitaji muhimu ya chakula na usafi kufanyika ndani ya
Wilaya ya Namtumbo na kukuza uchumi wa jamii hiyo.
Aidha, Dkt. Kiruswa amekagua maendeleo ya mradi wa uchimbaji
Madini ya Urani katika mgodi wa Mantra ambapo ameridhishwa na maendeleo ya
mradi na kuahidi kushughulikia mikwamo iliyopo kwa haraka ili uzalishaji wa madini
hayo uanze kama inavyo tarajiwa.
Naye, Meneja wa Uendelevu Mradi wa Mantra, Majani Wambura
amesema mpaka sasa mradi huo umetumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 240
katika ujenzi wa mradi na inategemewa mpaka kukamilika kwake dola za Kimarekani
zaidi ya bilioni moja zitatumika na ajira zaidi ya 700 zitatengenezwa kwa
jamii.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa ametatua na kumaliza
mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya Kampuni ya Mantra na Kikundi cha Kuza
Uchumi wa Namtumbo (KUNA) ambacho kinadai fidia ya eneo ulipo mradi kwasasa,
wakidai kuwa eneo hilo lilikiwa linamilikiwa na babu zao ambao waliondolewa kwa
nguvu na Wakoloni kati ya mwaka 1940 - 1945 na baadae eneo kutwaliwa na
Serikali na kulifanya kuwa hifadhi ya Taifa.
Dkt. Kiruswa amesema fidia ni haki ya Kisheria kwa mtu atakaye
hamishwa katika eneo lake kupisha mradi, hata hivyo, madai ya fidia ya Kikundi
hiki hayana msingi thabiti wa Kisheria kama ulivyo wasilishwa, hivyo
amewashauri wanakikundi hao kuangalia kwa upana faida watakazo nufaika nazo kwa
uwepo wa mradi huu ikiwa ni pamoja na fursa ya Kisheria ya wajibu wa Mmiliki wa
Leseni kwa Jamii (CSR) pamoja na Ushiriki wa Watanzania kwenye Uchumi wa Madini
(Local Content).
Aidha, Dkt. Kiruswa amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za
madini Mkoani humo ambapo ameupongeza Mkoa huo kwa kuvuka malengo ya makusanyo
ya maduhuli ya Serikali kwa asilimia 119 katika robo ya kwanza ya Mwaka wa
Fedha 2024/25.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Abbas
amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kufanya ziara Mkoani humo na kuahidi kuyafanyia
kazi maelekezo yote yaliyotolewa.
Awali, Dkt. Kiruswa aliungana na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa kukagua ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege inayoendelea Mkoani humo iliyoghalimu kiasi cha shilingi bilioni 37 ambapo maboresho yaliyofanyika ni pamoja na jengo la kuongoza ndege, uzio wa uwanja, taa za kuongoza ndege, eneo la urukaji wa ndege na lami katika barabara za uwanja wa ndege.
0 Maoni