WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutierres
kwenye Makuu ya umoja huo na kujadiliana masuala kadhaa yakiwemo ya maendeleo
ya jamii, ulinzi na usalama, siasa na ushirikiano wa Tanzania na UN.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wao jana (Jumamosi, Septemba 21,
2024), Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), amesema
katika suala la maendeleo ya jamii wamejadiliana umuhimu wa kuinua uwezo wa
wananchi kiuchumi ikiwemo upatikanaji wa huduma zote muhimu.
Kuhusu
ulinzi na usalama, Waziri Mkuu amesema Tanzania imepongezwa kwa kusimamia
ukombozi wa nchi nyingi za Afrika hasa za SADC. “Sasa hivi Serikali yetu
inaendelea kuunga mkono kwa kupeleka vikosi vya ulinzi kwenye nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki na za SADC,” amesema.
“Katika
hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amempongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan, wananchi na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha bara la
Afrika linabaki kuwa salama.”
Kuhusu
siasa, Waziri Mkuu amemweleza Katibu Mkuu huyo juu ya uwepo wa uchaguzi wa Serikali
za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao na
kusisitiza haja ya mtu kushiriki uchaguzi huo na haki ya kuchaguliwa.
Kwa upande
wake, Katibu Mkuu ameipongeza Tanzania kwa jinsi ilivyoshiriki kuisaidia
Burundi kuwa salama kwa kuendelea kuwapokea wakimbizi katika kipindi chote cha
nyuma. “Amesema ameridhishwa na hali ya usalama iliyopo ndani ya nchi hiyo, na
akashauri wakimbizi waanze kurejea nchini mwao ili waende kuijenga nchi yao na
kushiriki kwenye masuala ya maendeleo.”
Loe
(Jumapili, Septemba 22, 2024), Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki ufunguzi rasmi
wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) ambako atajumuika
na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa 193 na pia atatoa salamu za
Serikali.
Kaulimbiu ya
mkutano wa mwaka huu ni “Hakuna kuachwa nyuma yeyote: Kushirikiana pamoja
kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa
na vijavyo” (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of
peace, sustainable development and human dignity for present and future
generations).
0 Maoni