Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo
Tanzania (WMA), Albogast Kajungu, amesema WMA ina mchango mkubwa katika sekta
ya kilimo hususani katika mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, ufuta, kahawa,
tumbaku na pamba.
Amebainisha hayo Agosti 3, 2024 wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo maarufu kama NaneNane
yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa kazi kubwa ya Wakala wa Vipimo katika sekta
hiyo ndogo ya mazao ya kimkakati ni kuhakikisha Mizani zinazotumika katika
ununuzi wa mazao hayo zinahakikiwa ili kujiridhisha kuwa ziko sahihi.
“Lengo ni kuhakikisha kwamba mkulima anapouza mazao yake
anapata thamani ya pesa sawasawa na mazao aliyouza,” amefafanua Kajungu.
Akieleza zaidi, Mkurugenzi huyo wa Huduma za Ufundi amesema
zoezi la kuhakiki Mizani hufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza
huhusisha uhakiki wa mizani kabla ya msimu wa kila zao kuanza ilhali awamu ya
pili huhusisha ukaguzi wa kushtukiza wakati wa msimu kwa kila zao ili
kujiridhisha kama vipimo vilivyohakikiwa awali vinatumika kwa usahihi.
“Kwahivyo kabla ya msimu tunapita kuhakiki mizani zote
zinazotumika kununulia mazao na wakati wa msimu tunapita kujiridhisha kama
zinatumika kwa usahihi.”
Aidha, Kajungu ameeleza kuwa, mbali na zoezi la ukaguzi,
Wakala wa Vipimo pia hutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili
wafahamu sifa za mizani ya kununulia mazao iliyohakikiwa.
Ametaja mojawapo ya sifa za mizani iliyohakikiwa kuwa ni
uwepo wa stika ya Wakala wa Vipimo inayoonesha tarehe ambayo mizani husika
ilihakikiwa pamoja na tarehe ya mwisho ambayo stika hiyo itakuwa imekoma
matumizi yake.
“Kwahiyo mwananchi akiiona ile stika inampa uhakika kuwa
mizani hiyo imehakikiwa na Wakala wa Vipimo,” amesisitiza Kajungu.
Vilevile, akizungumzia kuhusu ufungashaji wa mazao ya
shamba, ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, kufungasha mazao ya shamba kwa
uzito unaozidi kilo 100 unatafsiriwa kama lumbesa ambayo ni kosa kisheria.
Amesema, kumekuwa na mkanganyiko wa tafsiri ya neno lumbesa
ambapo baadhi huitafsiri kama kufungasha mazao ya shamba kwa kuongeza kishungi,
ambapo tafsiri hiyo siyo sahihi.
Kajungu ametoa wito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla
kufahamu kwamba mazao yote ya shamba ni lazima yafungashwe kwa uzito
unaokubalika kisheria ambao ni kilo 100.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya vipimo,
Kajungu amesisitiza umuhimu wa kuwepo vituo vya kununulia mazao ambavyo ni
rahisi kuweka mizani iliyohakikiwa na WMA ili itumike kwa wakulima kuhakiki
mazao yao na kujiridhisha kwamba yamefungashwa katika uzito wa kilo 100 bila
kuzidi ili kupata faida stahiki kwa pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi.
Wataalamu wa Wakala wa Vipimo wanashiriki katika Maonesho ya NaneNane kitaifa jijini Dodoma na kikanda katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla.
Afisa Vipimo Mwandamizi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Said Ibrahim akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuhakiki dira za maji katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane (2024) yanayoendelea jijini Dodoma.Veronica Simba na Paulus Oluochi- WMA
0 Maoni