Ushiriki wa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa kivutio
kikubwa katika maonesho ya 30 ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Nane
Nane yanayoendelea kufanyika kitaifa Jijini Dodoma katika viwanja vya Nzuguni.
Uwepo wa vivutio vya wanyamapori hai, utambulisho wa banda
(branding) pamoja na vivutio vya Screen kubwa ya utangazaji kwenye magari ya
TANAPA, na shughuli za kiutamaduni kupitia gari la Makumbusho ya Taifa vimekuwa
vikiwavutia wananchi wengi kutembelea banda hilo. Aidha, washiriki kutoka Idara
na taasisi chini Wizara wamejipanga kutoa elimu ya uhifadhi na utalii pamoja na
kuhamasisha wananchi kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii nchini.
Akizungumza kwenye maonesho hayo ndani ya Banda la Wizara,
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Maendeleo ya Utalii ambaye pia, ni
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi kwa upande wa wizara, Bw. Juvenile Jaka
Mwambi, amesema ‘’ukifika kwenye banda hilo mbali na wanyamapori hai, pia
utajifunza na kuelezewa fursa mbalimbali za uwekezaji ndani ya Sekta ya maliasili
na Utalii pia utapata chakula cha aina mbalimbali ikiwemo nyamachoma ya
wanyamapori.’’
Amesema pia kuna makumbusho inayotembea ambayo itafanya
wananchi kujifunza mambo mbalimbali ya kale.
"Tunawakaribisha sana wananchi kuja kujifunza mambo
mengi ambayo hutaweza kuyapata kirahisi lakini kwenye maonesho haya ya Nanenane
utayapata."
Kwa siku ya leo, watu mbalimbali wametembelea banda hilo
akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Bi. Bure
Nassibu pamoja na Mkurugenzi wa Mafunzo na Takwimu, Dkt. Edward Kohi.
Vilevile, kwa mujibu wa taarifa za takwimu za wananchi waliotembelea banda la Wizara kwa siku ya ya leo kwa ujumla, wananchi 3,053 wamembelea banda hilo, ambayo ni idadi kubwa kuliko ya waliotembelea siku ya jana ambayo ni wananchi 813 sawa na ongezeko la asilimia 73 suala ambalo linaonesha namna gani Wizara hiyo imeendelea kuwa kivutio katika maonesho hayo.
Na. John Bera- Dodoma
0 Maoni