Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA)
Mohammed Simai amefanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara kwa lengo la
kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA)
ambapo amekiri kunufaika zaidi ya alivyotarajia.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake, Agosti 17, 2024
Simai amesema lengo hasa la ziara hiyo lilikuwa kutembelea eneo linalotumiwa na
Wakala wa Vipimo Mtwara kwa ajili ya ukaguzi na uhakiki wa magari ya
kusafirishia mafuta ili ZAWEMA ikatumie teknolojia hiyo na kuboresha zaidi huko
Zanzibar.
“Hata hivyo, ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwetu
kwa sababu tumepata zaidi ya kile tulichokusudia,” amesema.
Akifafanua, Simai ameeleza kwamba mbali na kujionea na
kujifunza kuhusu uanzishaji wa mtambo wa ukaguzi na uhakiki wa magari ya
kusafirishia mafuta, amepata fursa ya kutembelea maeneo mengine ambako WMA
hutekeleza majukumu yake ikiwemo Bandari ya Mtwara na katika eneo ambalo gesi
asilia huvunwa na kuchakatwa huko Madimba.
Amesema, matarajio yake ni kwenda kuibua miradi mbalimbali
ukiwemo wa ujenzi wa eneo la ukaguzi wa magari ya mafuta ambao utaenda sanjari
na ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa dira za maji kwa njia ya
kielektroniki. “Hata hivyo kwa nilichokiona huku WMA Mtwara, iko haja kutumia
mtambo wa kawaida pia pamoja na uwepo wa huo wa kielektroniki,” ameeleza.
Simai amemshukuru Mtendaji Mkuu wa WMA Tanzania Bara, Alban
Kihulla kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa ZAWEMA katika kuhakikisha
wanatimiza matarajio yao ya kutekeleza majukumu ya uhakiki vipimo kwa ufanisi
na tija kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Awali, akieleza kuhusu majukumu yanayotekelezwa na WMA
mkoani Mtwara, Meneja wa Mkoa wa Wakala hiyo, Saad Haruna amesema ni pamoja na
uhakiki wa vipimo ambavyo hutumika katika sekta za kilimo, biashara, mazingira
pamoja na usalama.
Katika sekta ya kilimo, Haruna amesema WMA huhakiki mizani
zinazotumika wakati wa kununua mazao pamoja na wakati wa kuyasafirisha.
Aidha, kwa upande wa biashara amesema WMA inawajibika
kuhakiki vipimo vinavyohusiana na sekta hiyo ambapo ametoa mfano wa mafuta
yanayosafirishwa kutoka nchi za nje kuletwa nchini kupitia Bandari ya Mtwara.
“WMA hufanya uhakiki kuanzia Bandarini mafuta yanaposhushwa
na kupita kwenye kipimo maalum kijulikanacho kama ‘flow meter’ kwa lugha ya
kigeni, zoezi ambalo huendelea kufanyika katika matenki ya kuhifadhi mafuta,
vituo vya mafuta na katika pampu zinazotumika kujaza mafuta katika magari.”
Vilevile, Haruna amesema jukumu lingine ambalo hutekelezwa
na WMA mkoani humo ni kuhakiki dira mpya za maji ambazo hutumika kuwafungia
wateja maji pamoja na zile ambazo zilikwishaanza kutumika.
Pia, katika sekta ndogo ya gesi asilia, amesema WMA
huwajibika kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kupima kiwango cha nishati hiyo
kuanzia inapovunwa hadi kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na hata kile kinachopelekwa kwa Kampuni
kubwa ya kuzalisha saruji ya Dangote.
Akizungumzia malengo ya kuhakiki vipimo, Haruna amesema ni
jukumu la Serikali kupitia Wakala wa Vipimo, kuhakikisha pande zote zinalindwa
yaani mlaji apate bidhaa kadri alivyolipia bila kupunjwa ilhali muuzaji apate
malipo stahiki kulingana na kiwango alichouza.
Kwa upande wake, mmoja wa Wasimamizi wa Mtambo wa kuchakata
gesi asilia katika Kiwanda kilichoko Madimba, Mussa Kongola ameipongeza
Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Vipimo akisema inatekeleza majukumu muhimu
sana yanayozinufaisha pande zote.
“Uwepo wa jicho la tatu ni muhimu sana ili kuhakikisha pande
zote zinanufaika kwa kupata kilicho stahiki na kwakweli nimewafahamu WMA kwa
muda mrefu, kazi yao ni njema sana,” amesisitiza.
Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa takwimu kutoka TPDC,
asilimia 60 ya umeme unaozalishwa nchini kupitia TANESCO hutokana na gesi
asilia. Aidha, korosho ambazo huzalishwa kwa wingi mkoani Mtwara ni moja ya
mazao ya kimkakati yanayolimwa nchini.
Vilevile, uwepo wa
Bandari ya Mtwara pamoja na maeneo mengine mbalimbali ambayo yanatumia vipimo,
vyote vinadhihirisha umuhimu wa uwepo wa Wakala wa Vipimo kwa manufaa ya uchumi
wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Utendaji mzuri wa wataalamu wa Wakala wa Vipimo Tanzania
Bara umekuwa ukivutia nchi mbalimbali kuja kujifunza namna bora ya kuendesha
sekta hiyo.
Ziara ya mafunzo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar imefanyika mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam au Mkoa mwingine kulingana na ukubwa wa kazi zinazotekelezwa na ZAWEMA ambao unaelezwa kuwiana na majukumu yanayotekelezwa na WMA Mtwara.
Gari lililobeba makaa ya mawe likipimwa uzito katika Bandari ya Mtwara kwa kutumia Mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA). Taswira hii ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Veronica Simba- WMA
0 Maoni