WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watoa huduma za
afya wa nchi wananchama wa kanda ya Afrika Mashariki kuondoa vikwazo
vinavyozuia wagonjwa wanaotafuta matibabu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
"Hatua hii ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa
uchumi wa kikanda na ukuaji wa utalii tiba."
Ametoa wito huo jana alipokuwa mgeni
rasmi katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika
Mashariki uliofanyika katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Njerere (JNICC) Dar es Salaam.
Amesema nchi wananchama ikiwemo Tanzania zimejitahidi
kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya
Kanda kwa matibabu.
"Kwa sasa ni wagonjwa wachache sana wanaosafiri nje ya
nchi zetu kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa
yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki,” alisema Mhe. Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa
wawekezaji wa Sekta ya Afya kuwekeza nchini Tanzania.
Amesema Serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji
hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini.
"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza
kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo,
mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate
teknolojia mpya na huduma za kibingwa."
Kadhalika amewataka wadau wa afya wa kanda kujadili mbinu
mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya na kuwa na mikakati ya pamoja ya
kukabiliana na magonjwa.
"Tumieni jukwaa hili kuweka mikakati ya pamoja ya
kupambana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza
pamoja na magonjwa mapya yanayotokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi,"
alisema Mhe. Majaliwa.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel
amesema uwekezaji uliofanywa na serikali kuanzia ngazi ya chini umewezesha
ugunduaji wa magonjwa yakiwa katika hatua za awali.
"Rufaa kwenda nje ya Nchi zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi cha nyuma watu waliokuwa wanafika Ocean Road walikuwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa, lakini kutokana na uwekezaji sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanakuja wakiwa na magonjwa katika hatua za awali," alisema Dk. Mollel.
0 Maoni