TIRA yaendelea na utoaji elimu ya Bima wilaya ya Magharibi

 

Ujumbe kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ukiongozwa na Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Said umeendelea na ziara yake ya kuelimisha kuhusu matumizi ya bima na leo hii Agosti 15, 2024 umezuru ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi na kutoa elimu kwa Masheha zaidi ya 65.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Mhe. Hamida Mussa Khamis ameipongeza TIRA kwa hatua ya kukutana na viongozi hao wa wananchi na kuwapa elimu muhimu ya bima hasa bima ya afya na kuwasihi Masheha kuwa mabalozi wazuri kwenye Shehia zao.

Nae Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Saidi amesema kuwa, lengo la Mamlaka ni kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora za bima na hivyo kuwataka wananchi hao wanapopata changamoto kuwasiliana na TIRA kupitia Kanda mpya ya Unguja inayohudumia mikoa yote ya Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.

Kwenye ziara hiyo TIRA pia imeambatana na Meneja anayeshughulikia maswala ya sheria kutoka Mfuko wa Bima ya Afya wa Zanzibar ambae aliwaelewesha Masheha hao juu ya umuhimu wa bima ya afya na namna ambavyo wananchi wanahudumiwa kupitia bima hiyo ikiwemo kutokua na ukomo wa kuhudumia watoto au wenza. TIRA kwa Soko Salama la Bima.



Chapisha Maoni

0 Maoni