Mloganzila kufanya tena kambi maalum ya upandikizaji wa nyonga na magoti

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeandaa kambi maalum ya ubingwa bobezi ya upasuaji wa upandikizaji nyonga na magoti bandia ambayo itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 26 hadi 30 Agosti, 2024, kambi hiyo itatanguliwa na zoezi la uchunguzi wa awali wa nyonga na magoti ambao utafanyika kuanzia tarehe 14 hadi 23 Agosti 2024.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Mifupa ambaye amebobea katika upasuaji wa nyonga na magoti MNH-Mloganzila, Dkt. Joseph Amos amesema kambi hiyo itafanyika kwa kushirikiana na jopo la madaktari wabobezi katika eneo la upandikizaji wa nyonga na magoti bandia watakaongozwa na Dkt. Venuthuria Ram Mohan Reddy kutoka nchini India ambaye ana uzoefu katika eneo la nyonga na magoti kwa zaidi ya miaka 20.

“Sio mara ya kwanza kwa Muhimbili Mloganzila kufanya kambi hii ya upandikizaji wa nyonga na magoti bandia kwani mwezi Novemba, 2023 tuliendesha kambi kambi kama hii ambapo ilipata mwitikio mkubwa na wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali walifanyiwa uchunguzi na hatimaye kupata matibabu ambapo kwa sasa wameondokana kabisa ya changamoto za maumivu ya nyonga na magoti,” amebainisha Dkt. Amos.

Dkt.  Amos ameongeza kuwa kambi hiyo inafanyika kutokana na mahitaji ya wananchi walio wengi ambao wengine hawakupata nafasi ya kupata huduma katika kambi iliyofanyika mwezi Novemba, 2023, hivyo ametoa rai kwa mwananchi yeyote anayehisi maumivu ya nyonga na magoti au ameshabaini ana tatizo la nyonga na magoti kujitokeza kufanyiwa uchunguzi na hatimaye matibabu.

Kwa wale watakaotaka kupata maelezo zaidi ya kambi hii wanaweza kuwasiliana na Dkt. Joseph Amos 0683680522, Dkt. Shilekirwa Makira 0765958302 au Dkt. Abubakar Hamis 0715219175.

Chapisha Maoni

0 Maoni