Watanzania wameaswa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwa kuchagua viongozi wanaofaa na
watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31, 2024 jijini Dodoma na Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati aliposhiriki
bonanza la michezo la Bunge lililokuwa na kauli mbiu inayosema shiriki uchaguzi
kwa maendeleo ya Taifa.
‘‘Bonanza hili liwe chachu ya kuwakumbusha Watanzania
umuhimu wa kuchagua viongozi wanaofaa kwa ajili ya kutuletea maendeleo katika
Taifa hili. Viongozi watakao tuunganisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali
bila kujali hali zao, dini zao, makabila yao wala vyama vyao vya siasa, bonanza
hili litukumbushe kuwa tunaenda kuchagua viongozi wanaofaa kwenye utawala wa
nchi hii, viongozi wa kitongoji au mwenyekiti wa kitongoji au kijiji hawa ni
viongozi muhimu wanaokaa na watu wakati wote tusiwachukulie poa wakati wa
uchaguzi huu, tuchague viongozi wenye uwezo,’’ amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua ‘‘Uongozi utakao chaguliwa uwe kutokana na sifa
na kampeni tusiruhusu kubaguana ama kutukanana badala ya kunadi sera zetu,
bonanza hili litukumbushe pia kuwa baada ya uchaguzi maisha yanaendelea na
maisha yataendelea tu kama tutachaguana kwa haki, upendo tukisisitiza umoja wa
kitaifa na muungano wetu.’’
Vilevile, Dkt. Biteko ameipongeza Benki ya NMB kwa kuunga
mkono juhudi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchangia kiasi
cha fedha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya
Wavulana ya Bunge.
‘‘Nampongeza Spika wa Bunge kwa kufanya ubunifu wa kuwa na
Bunge Bonanza ambalo limeleta mageuzi makubwa, kuonesha utu na kufanya
wabunge wafurahie kazi yao na kuruhusu
vipaji ili kuwa na Bunge Sports Club pamoja na Bunge Bonanza. Nawapongeza pia
waheshimiwa wabunge wote kwa kushiriki michezo mbalimbali katika bonanza
hili,’’ amemaliza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani
(IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameishukuru Benki ya NMB kwa kuwa wadau wa karibu
wa Bunge na wabunge ambao wamekuwa
wakishirikiana kwenye maeneo yao mbalimbali na kuwa bonanza hilo ni mojawapo tu, aidha kupitia ushirikino huo NMB imetoa mchango wao maalum kwa ajili ya
kuunga mkono juhudi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga
Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bunge.
‘‘Shule hii inajengwa
kwa kuwa Bunge lilishajenga Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Bunge na sisi tunatambua kwamba watoto wa kike lazima
wapate elimu iliyo bora na watoto wetu wa kiume pia wapate elimu iliyo bora na
hivyo tumejenga shule bora ya wasichana na tunajenga ya wavulana na hiyo hii
itakuwa imeweka uwiano sawa kuwa Bunge
tunathamiani watoto wa kike na wakiume,’’ amesema Dkt. Tulia.
Pia, ametoa wito kwa wadau wengine kuwa kuendelea kutoa
michango yao ili ujenzi wa shule hiyo
ukamilike kwa wakati.
Naye, Mwakilishi wa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
Mhe. Yahya Rashid Abdulla amesema kuwa Baraza la wawakilishi litaendeleza
ushirikiano uliopo katika kati ya mabunge hayo mawili.
Mwenyekiti wa Bonanza la Bunge Mhe. Festo Sanga amesema
‘‘Spika alielekeza Bunge lifanyekazi kama taasisi hivyo ni muhimu kuwa na
ushirikiano na taasisi zingine na leo katika bonanza hili tumeshirikiana na
Wizara ya Maji, Nishati na Benki ya NMB, ’’ amesema Mhe. Sanga.
Vilevile, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB,
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw Juma Kimori amesema kuwa Bunge limekuwa
likishirikiana na NMB kwa masuala ya kifedha na kuwa wanawashukuru wabunge kwa
kuendelea kutumia huduma zao pamoja na kushirikiana na benki hiyo katika
majimbo yao.
‘‘Katika programu
zetu za kurudisha kwa jamii tumekuwa tukishirikiana katika elimu, afya na
masuala mbalimbali, NMB itaendelea kushirikiana na nyie katika kuleta maendeleo
katika maeneo mbalimbali, NMB imejikita
katika kuleta suluhisho kwa jamii yetu na sasa tuna programu ya kuhakikisha
tunafika katika kila kijiji Tanzania
mfano mikopo mshiko fasta ni mkopo unaomlenga mwananchi ambao hauna
masharti kama mikopo mingine, ’’ amesisitiza.
Awali Dkt. Biteko ameshiriki bonanza la Bunge katika matembezi kutoka Chuo cha Mipango hadi Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini na baada kutoa zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akimvisha medali Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson wakati aliposhiriki bonanza la michezo la Bunge lililokuwa na kauli mbiu inayosema shiriki uchaguzi kwa maendeleo ya Taifa.
0 Maoni