Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa Mikumi imeleta mafanikio makubwa katika Sekta ya Utalii nchini yakichangiwa na jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana
(Mb) wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani
Morogoro ambapo amesema kupitia filamu
maarufu ya “Tanzania: The Royal Tour” pamoja na filamu ya “The Amazing TANZANIA”zimekuwa
chachu ya kukuza utalii na kuongeza idadi ya wageni wa ndani na nje ya nchi.
“Kufuatia jitihada hizo za Rais Samia, katika mwaka wa fedha
2023/2024 idadi ya watalii wa kimataifa waliofika nchini imeongezeka kwa
asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,808,205
Mwaka 2023,” amesisitiza Mhe. Chana na kuongeza kuwa upande wa Hifadhi ya Taifa
Mikumi, kwa mwaka 2023/2024 jumla ya watalii 138,844 wametembelea Hifadhi hiyo
sawa na ongezeko la asilimia 198.48 kutoka watalii 46,517 waliotembelea hifadhi
hiyo kwa mwaka 2020/2021.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa
watalii kwa kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya
mwendokasi (SGR), kuimarisha Shirika la Ndege nchini (ATCL) na ujenzi wa
barabara kurahisisha watalii kufikia vivutio mbalimbali.
Katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya Hifadhi ya
Taifa Mikumi, Serikali kupitia Mradi wa REGROW inaboresha uwanja wa ndege kuwa
wa kisasa katika eneo la Kikoboga, ujenzi wa malango ya watalii eneo la Doma na
Kikwaraza, ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa kwa wageni (VIC), kambi za
kupumzikia wageni (Picnic Sites), maeneo ya malazi (Cottages & Campsites)
na kuunganisha Hifadhi ya Taifa Mikumi kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.
Amesema miradi hiyo itakapokamilika itawezesha kuongeza
idadi ya watalii kwa kuwa ndege kubwa zaidi zitaweza kutua ndani ya Hifadhi ya
Taifa Mikumi ambapo kwa wakati mmoja wageni zaidi ya 140 wataweza kuhudumiwa
kwa pamoja.
Pia, amesema Serikali imepanga kujenga lango la kupokelea
watalii watakaokuja Mikumi kwa njia ya reli ya ya kisasa ya mwendokasi (SGR)
kupitia kituo cha reli ya SGR kilichopo kwenye mji wa Kilosa. Ujenzi wa lango
hili utaleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya Kilosa hususan kwa
vijiji vya Myombo, Mbamba na Kilangali.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA), Musa Kuji amesema kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilikua
ikishika nafasi ya 14 kati ya hifadhi 21 katika ukusanyaji wa mapato ambapo kwa
sasa iinashika nafasi ya 6.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna
Msaidizi wa Uhifadhi, Augustine Massesa
amesema kupitia utalii wa Hifadhi ya Taifa Mikumi uchumi wa jamii
zinazozunguka eneo hilo umeongezeka, wameweza kushirikiana na jamii kuwapa fursa
za ajira, elimu ya uhifadhi, miradi ya maendeleo pamoja na kushirikiana na
Askari wa Vijiji (VGS) kukabiliana na changamoto ya Wanyamapori wakali na
waharibifu.
Hifadhi hii ni hifadhi kongwe ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya tano kuanzishwa baada ya Hifadhi za Taifa za Serengeti (1951), Ziwa Manyara (1960), Arusha (1960) na Ruaha (1964), inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na 465.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) akikata keki maaluma wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani Morogoro.
0 Maoni