Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kutumia fursa ya
Sherehe za Wakulima, Wavuvi na Wafugaji zilizopangwa kufanyika Eneo la Nzuguni,
Jijini Dodoma tarehe 01 hadi 08 Agosti, 2024 kutangaza utalii wa ndani kwa
kuhamasisha uwekezaji na wananchi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo
mkoani Dodoma na maeneo ya karibu.
Akizungumza kwenye Kikao cha Maandalizi ya Maonesho hayo, Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi kwa upande wa Wizara, Bw. Emmanuel Msoffe amesema
Wizara imejipanga kuhakikisha inatangaza vivutio vya utalii vilivyopo maeneo
mbalimbali nchini, kuhamasisha shughuli za uwekezaji kwenye sekta ya utalii,
maliasili na malikale pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kutembelea maeneo ya
vivutio vinavyosimamiwa na taasisi zake za Uhifadhi kwa utaratibu maalum.
Amesema ‘’Sherehe za Nanenane kwa mwaka huu zinazafanyika
Jijini Dodoma ambapo zitafunguliwa na kufungwa na viongozi wakubwa wa kitaifa,
hivyo, Wizara inaendelea kujipanga vizuri kushiriki kikamilifu katika kutangaza
utalii hususan utalii wa ndani.’’
Kwa kawaida, Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali
ya utangazaji utalii ambapo maonesho na matukio (MICE) kama Sherehe za
‘Nanenane’ ni fursa muhimu katika utangazaji utalii. Jitihada hizo zinaenda sambamba na kuunga
mkono azma ya Serikali ya kufikia idadi ya watalii milioni 5 na mapato
yatokanayo na utalii Dola za Marekani bilioni 6.
Sherehe za Wakulima, Wavuvi, na Wafugaji hufanyika kila
mwaka ambapo kitaifa hufanyika kwa mzunguko katika Kanda mbalimbali ambapo kwa
mwaka huu, 2024, kitaifa zitafanyika Jijini Dodoma.
Sherehe hizo
zinalenga kutambua mchango wa sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji katika ukuaji
wa uchumi, kuwakutanisha wadau wa sekta husika kubadilishana uzoefu na kuonesha
shughuli na fursa zilizopo kwenye sekta hizo. Mgeni Rasmi wakati wa kilele cha
sherehe hizo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Sekta za Maliasili na Utalii ni sekta muhimu zinazofungamanishwa kwenye sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji ili kuimarisha mnyororo wake wa thamani. Hivyo, Wizara, taasisi chini ya Wizara na wadau wa sekta binafsi za utalii na maliasili wanatarajiwa kushiriki sherehe hizo.
Na. John Bera- Dodoma
0 Maoni